Polisi wakanusha Besigye alitekwa nyara Kenya lawama zikiongezeka dhidi ya serikali
MKE wa Kiongozi wa Upinzani nchini Uganda Kizza Besigye amelitaka jeshi la Uganda kumwachilia mumewe anayezuiliwa katika korokoro lao jijini Kampala.
Kulingana na Bi Winnie Byanyima, Dkt Besigye amefungiwa baada ya kutoweka Jumamosi akiwa jijini Nairobi, Kenya ambako alikuwa anahudhuria uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua.
Bi Byanyima anadai kuwa mumewe alitekwa nyara na watu wasiojulikana na ambao aliwashuku kuwa maafisa wa usalama.
Hata hivyo, Msemaji wa Polisi nchini Kenya Dkt Resila Onyango amekana madai kuwa Besigye, ambaye ni kiongozi wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC), alitekwa nyara Kenya.
“Naiomba serikali ya Uganda imwachilie huru mume wangu Dkt Kizza Besigye mara moja. Alitekwa nyara Jumamosi iliyopita akiwa Nairobi kuhudhuria uzinduzi wa kitabu cha Mhe Martha Karua,” Bi Byanyima akaandika katika akaunti yake ya mtandao wa X Jumatano, Novemba 20, 2024, asubuhi.
“Sasa nimefahamishwa kwamba anazuiliwa katika gereza moja la jeshi jijini Kampala. Sisi kama familia na mawakili wake tunataka kumfikia. Yeye sio mwanajeshi. Mbona anazuiliwa katika gereza la wanajeshi?” Bi Byanyima, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi (UNAIDS) akauliza.
Amewahi kuwania urais mara nne
Dkt Besigye, ambaye amewahi kuwania urais mara nne, alionekana mara ya mwisho Jumamosi jioni katika nyumba moja ya makazi mtaa wa Riverside Drive eneo la Westlands, Nairobi.
Mwanasiasa huyo alikuwa amekodishiwa chumba katika mkahawa ya Waridi Paradise Hotel and Suites mtaani Hurlingham, ambao hauko mbali na Riverside Drive.
Mhudumu katika mkahawa huo aliambia gazeti la The Monitor Jumanne jioni kuwa Besigye hakuwa amerejea humo tangu alipoondoka Jumamosi.
Kisa cha kutoweka kwa Besigye kinajiri miezi mitano baada ya wanaharakati 36 kutoka Uganda, wenye uhusiano na mwanasiasa huyo, kukamatwa jijini Kisumu.
Baada ya kukamatwa kwao Julai 23, 2024, wanaharakati hao walisafirishwa hadi Uganda ambako walishtakiwa kwa uhaini na kuzuiliwa katika rumande ya Kitalya.
Wanaharakati hao, ambao juzi waliachiliwa huru kwa dhamana, walikana mashtaka hayo na kusema walikuwa wakihudhuria warsha fulani Kisumu walipokamatwa.
Walidai kuwa waliteswa wakiwa kuzuizini.
Uchaguzi wa urais umeratibiwa kufanyika nchini Uganda mnamo Septemba 2026 ambapo Rais wa sasa Yoweri Museveni ameapa kutetea kiti chake.
Museveni ameongoza Uganda kwa zaidi ya miaka 40, tangu 1986 na ni mmoja wa marais wa Afrika ambao wamesalia uongozi kwa miaka mingi zaidi.