Besigye kortini; ashtakiwa kwa njama ya kulipua kambi za jeshi Uganda
MWANASIASA mkongwe wa upinzani wa Uganda Dkt Kizza Besigye aliyetoweka nchini Kenya Jumamosi na baadaye kudaiwa kutekwa nyara, ameshtakiwa nchini Uganda.
Aliwasilishwa katika mahakama moja ya kijeshi jijini Kampala mnamo Jumatano, Novemba 20, 2024, na kushtakiwa kwa makosa kadhaa likiwemo kosa la umiliki wa bunduki kinyume cha sheria.
Pia, alikabiliwa na tuhuma za kufanya mikutano katika nchi za Kenya, Uswizi na Ugiriki kwa lengo la kusaka uungwaji mkono wa kifedha na zana kwa lengo la kushambulia kambi za kijeshi nchini Uganda.
Ilidaiwa kuwa mipango hiyo inalenga kuhujumu usalama wa Jeshi la Uganda (UPDF).
Wakili wa Dkt Besigye Erias Lukwago alisema hati ya mashtaka ilikuwa na dosari.
“Kwa hivyo kesi hii ni batili,” akaambia shirika la habari la Reuters baada ya Dkt Besigye kukana mashtaka yote dhidi yake.
Kulingana na shirika hilo la habari, Dkt Besigye alisukumwa rumande ya gereza la Luzira hadi Desemba 2, 2024.
Awali, mkewe kiongozi huyo wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC), Winnie Byanyima alidai kuwa mumewe alitekwa nyara na maafisa wa usalama wa Uganda wakisaidiwa na wenzao wa Kenya.
“Ninaomba serikali ya Uganda imwachilie huru mume wangu Dkt Kizza Besigye kutoka korokoro ya kijeshi ambamo wamemzuilia. Yeye si mwanajeshi,” akasema kupitia mtandao wa X (zamani Twitter).
Dkt Besigye ambaye aliwasili nchini Kenya kwa ajili ya kuhudhuria uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na Bi Karua, alitoweka Jumamosi jioni katika jengo la 108 Riverside Apartment eneo la Westlands ambako ilisemekana alienda kukutana na ‘watu fulani.’
Alikuwa amekodisha chumba cha kulala katika mkahawa wa Waridi Paradise Hotel and Suites ulioko katika mtaa wa Hurlingham, Nairobi.
Kiongozi huyo wa upinzani Uganda alitarajiwa kuwa miongoni mwa wahutubu Jumapili Novemba 17, 2024 katika halfa ya uzinduzi wa kitabu hicho, “Against the Tide” kinachoelezea pandashuka za kisiasa za Bi Karua.