Makala

Jinsi sheria mpya zitakavyowakomboa bodaboda kutoka kwa mikopo ya kilaghai

Na MARY WANGARI November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MASAIBU ambayo waendeshaji bodaboda wamekuwa wakiyapitia mikononi mwa mashirika tapeli ya kutoa mikopo ya pikipiki, huenda sasa yakafika kikomo baada ya bunge la kitaifa kuanza rasmi mchakato wa kuzima kero hilo.

Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Fedha imekusanya maoni kutoka kwa wadau husika kuhusiana na pendekezo linalodhamiriwa kuwakomboa waendeshaji bodaboda kutoka minyororo ya wakopeshaji kidijitali.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo, Kimani Kuria, ilianzisha uchunguzi baada ya kupokea malalamishi kuhusu unyanyasaji unaotekelezwa na baadhi ya mashirika ya ukopeshaji kidjitali.

Waendeshaji bodaboda wanataka sheria zibuniwe kudhibiti sekta hiyo inayoruhusu malipo baadaye (BNPL), ambayo imekuwa ikiendeshwa bila kudhibitiwa.

Miswada mitatu inayotazamiwa kulainisha sekta hiyo na kuwalinda wahudumu wa bodaboda ni pamoja na Marekebisho ya Sheria kuhusu Ushuru 2024, Marekebisho ya Sheria kuhusu Kanuni za Ushuru 2024 na Marekebisho ya Sheria kuhusu Biashara 2024.

Endapo utapitishwa kuwa sheria, Mswada wa Marekebisho ya sheria kuhusu Biashara 2024, unaopendekeza kurekebisha Sheria kuhusu Benki Kuu ya Kenya (CBK), utasaidia kung’oa mashirika tapeli kwa kupiga marufuku utoaji huduma hizo bila leseni.

Ina maana kuwa mashirika yote ya ukopeshaji kidijitali ambayo hayakuwa yakidhibitiwa sasa yatadhibitiwa na CBK ambayo itabuni kanuni za utekelezaji huku watoaji huduma za ukopeshaji watakaokiuka sheria husika wakiadhibiwa.

Kupitia juhudi za Afisi ya Kamishna wa Data na CBK, mswada huo utaweka masharti yanayostahili kutimizwa na mashirika ya ukopeshaji kidijitali ili kulainisha sekta hiyo na kuwalinda wateja wanaonunua pikipiki kupitia mpango huo.

“Katika mchakato wa kulipisha deni au mkopo, biashara ya ukopeshaji haitahangaisha, kutusu, au kumkandamiza aliyekopa au mdhamini, wala kutishia, kutumia ukatili au lugha ya matusi,” unaeleza mswada huo.

Isitoshe, sheria hizo zinadhamiriwa kuimarisha uwazi kwa kushurutisha mashirika ya ukopeshaji kuweka wazi kupitia maelezo sahihi kuhusu masharti ya ukopeshaji na gharama za kifedha ambazo mteja atahitajika kutimiza ikiwemo kulinda maelezo ya siri wanayopatiwa na wateja.

Sheria hizo zinakusudiwa kuwalinda wateja kutokana na ukandamizaji kutoka kwa mashirika ya ukopeshaji ikiwemo kuweka masharti kwa wanaojihusisha na biashara hiyo, ada za kifedha zinazohusu mikopo, haki na wajibu unaohusu mikopo.