Habari za Kitaifa

Ruto afutilia mbali dili ya Adani  

Na SAMMY WAWERU November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ametangaza kufutilia mbali mpango wa Adani, ulionuiwa kutumika kukarabati Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), Jijini Nairobi.

Dkt Ruto ameonekana kuchukua hatua hiyo baada ya mwenyekiti wa Adani Group, Gautam Adani kushtakiwa New York, Amerika akihusishwa na kashfa ya ufisadi wa Dola 250 milioni (sawa na Sh32.4 bilioni thamani ya Kenya) ili kupata tenda ya kawi ya Dola 2 bilioni (Ksh259.2 bilioni).

Mpango wa Adani kukarabati JKIA, umekuwa ukikosolewa pakubwa.

Kwa mujibu wa dili ya Adani na serikali ya Kenya, uwanja huo mkuu nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ungesalia chini ya uongozi wa Adani kwa muda wa miaka 30, jambo ambalo limekuwa likiibua maswali chungu nzima.

Kampuni ya Adani ilikuwa imetoa ahadi ya Dola 1.85 bilioni (Ksh239.7 bilioni) kuwekeza JKIA.

Rais Ruto, kwenye hotuba yake kwa taifa Alhamisi, Novemba 21, 2024, alisema serikali itasaka mwekezaji mwingine kuboresha JKIA.