Tumekwama na mahindi, hatuna wanunuzi, wakulima sasa walilia Ruto
WAKULIMA wa mahindi kutoka kaunti mbalimbali wamekwama na mamilioni ya magunia ya mazao yao huku wakisema wameshindwa kupata soko.
Kwa mfano, katika eneo la North Rift, wakulima wamevuna magunia milioni 60 kutoka magunia milioni 41 ya mahindi mwaka 2023.
Kwa sasa, wanashutumu serikali ya Rais William Ruto kwa kushindwa kudhibiti bei ya mahindi na hata kuwalinda dhidi ya walaghai.
Wametoa wito kwa Rais Ruto kueleza wazi mipango ya serikali kuhakikisha mapato bora wakati wa mavuno, na kuhakikisha serikali yake inaweka fedha zaidi katika mpango wa kutoa mbolea ya ruzuku ili kuwafaidi zaidi mashinani.
“Tunamtaka Rais atuambie mipango yake kutuhusu. Mwaka huu tumeuza mahindi yetu kwa bei ya chini ya Sh 2,000 kwa gunia na hii haifai. Tunataka bei nzuri zaidi baada ya bidii yetu katika mashamba,” alibainisha mkulima wa Trans Nzoia Peter Kirwa.
Kwa sasa, wakulima hao wanaitaka serikali kununua mazao yao angalau kwa Sh4,000 kwa kilo 90 ili kuwasaidia kupata faida na kuwawezesha kuwekeza katika zao lijalo.
Aidha wanaitaka serikali kupitia upya Warehouse Receipt System (WRS), ambapo wanaweza kuhifadhi mazao yao wakisubiri bei ipande.
Haya yanajiri huku wakulima mkoani humo wakiachana na kilimo cha mahindi na kuanza kulima miwa, wakitaja faida duni kutokana na kilimo cha mahindi.
“Baadhi ya watu wetu wameacha kilimo cha mahindi ambacho ni tishio kwa usalama wa chakula. Serikali lazima iangazie suala hilo ili kuvutia wakulima zaidi katika kilimo cha mahindi,” akasema mkulima wa Trans Nzoia Kennedy Lutukai.
Walio katika skimu ya unyunyizaji maji ya Perkerra katika Kaunti ya Baringo wanalalamikia gharama ya juu ya uzalishaji ambayo imewasababishia hasara kubwa.
Wakulima pia wana wasiwasi kuhusu usambazaji ‘usioratibiwa’ wa pembejeo muhimu za kilimo, ambao unasababisha wakulima wadogo kukosa mahitaji.
“Serikali inahitaji kurahisisha mchakato wa ununuzi na usambazaji ili kuondoa makampuni ambayo yamejipenyeza kwenye biashara hiyo, kuwapa wakulima mbolea ghushi,” alisema Kipkorir Menjo, mkurugenzi wa Chama cha Wakulima Kenya (KFA).
Wengine walilalamikia gharama kubwa za uzalishaji, wakitaja hasara kubwa.
Bw Michael Bartonjo, mkulima katika skimu hiyo alisema ushuru wa juu umewakosesha raha, na kuwasababishia kupata zaidi ya Sh60,000 kwa uzalishaji kwa ekari moja ya mahindi.
“Tunataka kumwambia Rais Ruto kwamba ushuru wa juu umeathiri vibaya wakulima wa mahindi katika skimu ya unyunyiziaji maji ya Perkerra, na hivyo kuwafanya waishi kwa mikopo. Kutokana na hofu ya kupata mbolea ghushi ya ruzuku wakulima wengi walichagua kuzinunua katika maduka kwa gharama ya juu sana,” akasema Bw Bartonjo.
Ripoti za Evans Jaola, Barnabas Bii, Florah Koech, Sammy Lutta na Oscar Kakai
IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO