Makala

Mawaidha ya Kiislamu: Viongozi wa dini nyinginezo nao pia wajitokeze kukemea maovu

Na ALI HASSAN KAULENI November 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Tumejaaliwa leo hii, siku hii kubwa tukufu na aula ili kukumbushana kulihusu neno lake Mwenyezi Mungu.

Awali ya yote tuufungue ukurasa wetu leo hii kwa kumpwekesha na kumuenzi mmoja tu, Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo: Allah (SWT).

Katika uzi uo huo, tumtilie dua na kumfanyia kila aina ya maombi, mwombezi wetu, Mtume (SAW).

Ni yetu matumaini kuwa kwa kuandika makala haya, na kwa wewe kuyasoma, basi tuna imani na maombi kuwa Allah (SWT) ataneemesha zaidi hali zetu kutokana na ibada hii, na atujaalie mwisho mwema majaaliwa.

Leo hii ndugu yangu unayasoma makala haya huku vyombo vya habari, si runinga, si redio, si magazeti na hata mitandaoni kukiwa kumechacha! Kisa na maana? Majuzi wamejitokeza viongozi wa dini, makanisa hasa, wakasema kwa kauli moja.

Na ujuavyo kauli ya kiongozi yeyote yule wa dini huwa na msisimko, mashiko na uzito wa kutetemesha ardhi.

Je, i wapi kauli ya viongozi wa dini nyinginezo? Na hasa dini ya Kiislamu? Ukweli wa mambo ni kuwa baadhi ya viongozi wa dini hii tukufu ya Kiislamu wamekuwa wakikemea uhuni, unyama, udhalimu katika jamii kupitia maabadi kama misikiti na majukwaa mengineyo sikwambii kupitia vyombo vya habari.

Labda itabidi sasa kuonesha umoja na kujitokeza bayana tena kwa kinywa kipana kama walivyofanya viongozi wa makanisa.

Aidha, lipo baraza kuu la viongozi wa dini kote nchini. Yalikuwa matarajio yetu kuwa kauli hiyo ya viongozi wa makanisa, ingekuwa kubwa zaidi kama pia ingeandamana na kauli ya viongozi wa dini nyinginezo, hasa dini ya Kiislamu.

Wajua tena kimya chao kinaweza kutafsiriwa vinginevyo, au sio? Baada ya kimya cha muda tangu uongozi wa Kenya Kwanza kuchukua uongozi wa nchi, wananchi na waja kwa ujumla wamekuwa wakipiga nduru na mayowe lakini vyote hivyo vikimezwa na ukimya wa utawala.

Achia mbali maandamano ya vijana, Gen-Z, ambayo kwa kiasi kikubwa yalitikisa utawala uliopo mamlakani kwa sasa.

Kauli nzito ya majuzi ya viongozi wa dini imeisuta serikali kwa kuzembea kwingi tu na kufumbia macho kupanda kwa gharama ya maisha, kuongezeka kwa kila aina ya matozo (ushuru), changamoto zinazozikumba sekta ainati kama vile elimu na afya pasi kusahau ongezeko la idadi ya mauaji, utekaji nyara na kamata kamata za wale ambao wanadhaniwa kuikosoa serikali.

Je, kilio cha viongozi wa dini kitasikizwa?

LANGU JICHO!

Ijumaa Mubarak!