Afya na Jamii

Kinachosababisha kuvuja damu wakati wa ujauzito

Na PAULINE ONGAJI November 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

 

KUNA baadhi ya wanawake ambao hushuhudia damu kuvuja wakiwa wajawazito, suala linalowatia wasiwasi.

Ni kawaida kushuhudia hili hasa ikiwa damu hiyo ni matone tu.

Kuna mambo kadha wa kadha ambayo husababisha hali hii. Kwa mfano, kuvuja damu ukiwa mjamzito, wakati ambapo mimba inajitundika kwenye ukuta wa uterasi.

 Damu hii hutoka wiki za awali za ujauzito na kwa kawaida haitoki kwa wingi.

Aidha, unaweza kuvuja kutokana na mwasho kwenye lango la uzazi, au ikiwa kuna maambukizi, au ikiwa mimba imejitundika nje ya uterasi (ectopic pregnancy), au ikiwa kuna hatari ya mimba kutoka.

Kwa kawaida matatizo haya huhitaji kuangaliwa na mwanajinalokojia.

 Huenda uchunguzi wa maabara ukahitajika na wakati mwingine kupigwa picha ya sehemu ya nyonga.

Ikiwa mimba imejitundika nje ya uterasi na unavuja damu, basi upasuaji wa dharura hufanywa. Ikiwa ni mimba inatoka, utalazwa hospitalini upokee matibabu .

Wakati mwingine, kuvuja damu hutokana na kuwa tayari mimba inatoka na hivyo huenda ukapewa dawa au ukafanyiwa utaratibu wa kimatibabu.