KNEC yazima walimu ambao shule zilihusishwa na udanganyifu kusahihisha mitihani
NI pigo kwa baadhi ya walimu watahini nchini baada ya Baraza la kitaifa la mitihani nchini (KNEC) kuwatumia jumbe za kuwataka kutoshiriki zoezi la kusahihisha mitihani.
Walimu hao hawakuelezwa sababu ya KNEC kuwatumia jumbe hizo wiki hii licha ya wao kupokea barua za mwaliko hapo awali.
Taifa Leo imebaini kwamba walimu wote waliopokea jumbe za KNEC za kutohudhuria zoezi la usahihishaji ni wale ambao shule zao zilipatikana kuwa na dosari fulani wakati mitihani ya KCSE ilipokuwa ikiendelea. Hatua ya KNEC imezua tumbojoto miongoni mwa walimu wakuu wa shule nyingi za sekondari nchini.
Mtihani wa kidato cha nne ulikamilika rasmi Ijumaa Novemba 22, 2024. Serikali ilikuwa imeweka mipango kabambe kuzuia udanganyifu . Mojawapo ya mikakati hiyo ni karatasi za maswali kuwa na jina la mwanafunzi, nambari ya usajili ya mwanafunzi pamoja na jina na nambari fiche ya shule. Hatua hizi zilisaidia kupunguza usambazaji wa mitihani mtandaoni.
Vile vile hatua ya walimu watahini kutoka shule zilizohusishwa na dosari kwa njia moja au nyingine kuzuiliwa kusahihisha ni njia moja Baraza la mitihani limechukua kuzuia kuendeleza udanganyifu.
Usahihishaji wa mitihani ya KCSE unatarajiwa kuanza rasmi juma lijalo.