Habari Mseto

Wakili abubujikwa na machozi baada ya kuzabwa bondi ya Sh5 milioni Mombasa

Na LABAAN SHABAAN November 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKILI Sheila Nkatha Muthee alitiririkwa na machozi baada ya kuzabwa na bondi ya Sh5 milioni kuhusiana na kesi ya kashfa ya Sh17.5 milioni.

Bi Muthee anayefanya kazi ya uwakili jijini Mombasa alishtakiwa kwa makosa kadhaa pamoja na kuiba Sh17.5 milioni kutoka kwa mteja wake.

Mnamo Ijumaa, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mombasa Rita Orora aliamuru aachiliwe kwa dhamana ya Sh5 milioni na mdhamini wa kiasi sasa.

Katika uamuzi wake, Bi Orora alisema hakuwa na budi ila kusawazisha haki za mshtakiwa na za mlalamishi kwa mujibu wa sheria.

Awali kulitokea na hali ya suitafahamu kortini baada ya Bi Muthee, kupitia wakili wake Elijah Gathu, kufahamisha korti kuhusu kuwepo kwa maelewano ya kusuluhisha kesi nje ya mahakama.

“Kuna maelewano yanayoendelea kwa mshukiwa kulipa Sh1.5 milioni na tunangoja kibali cha mlalamishi kusuluhisha mzozo nje ya korti,” akasema Bi Muthee.

Alikuwa akiomba hakimu atoe uamuzi huo baadaye adhuhuri (Ijumaa) wakisubiri kesi iondolewe kortini na mlalamishi.

Lakini baadaye, Bi Muthee aliambia korti kuwa mlalamishi alidinda kuondoa kesi.

Upande wa mashtaka uliambia korti kuwa Bi Muthee aliiba pesa ambazo zilikuwa sehemu ya mapato yaliyotokana na mauzo ya mali ya kampuni ya Crispy Ltd.

Bi Muthee alipokea pesa hizo katika akaunti ya benki ya kampuni yake.   Anashukiwa kufanya kosa hilo siku tofauti kati ya Februari 17, 2024 na Julai 23, 2024 katika Kaunti Ndogo ya Mvita.

Vile vile, anakabiliwa na mashtaka kumi ya kutoa hundi mbovu.

Korti iliambiwa kuwa Bi Muthee aliandika hundi Julai 18, 2024 akiwa meneja mshirika wa Kampuni yake ya Muthee and Partners.

Alitoa hundi hiyo ya Sh900,000 kwa akaunti ya Benki ya Cooperative kwa manufaa ya Osman Mohamud Mohamed akijua akaunti yake haikuwa na pesa za kutosha.

Kongamano la kupanda vikao vya kusikiliza kesi hiyo limeratibiwa kuanza Desemba 9, 2024.