Habari Mseto

Mhudumu ashtakiwa kwa kubaka mgonjwa hospitalini

Na SIMON CIURI November 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MHUDUMU mmoja katika hospitali ya kibinafsi huko Kiambu ameshtakiwa kwa kumbaka mgonjwa mwanamke.

Mwanamke huyo, 26, alikuwa ametembelea Hospitali ya Plainsview huko Ruiru ili kupata ushauri wa daktari wa uzazi alasiri ya Jumamosi, Novemba 16.

Alilipa ada ya usajili  ya Sh2,000 na aliwekwa kwenye foleni kusubiri kuona mwanajinakolojia.

Daktari alimshauri afanyiwe uchunguzi zaidi. Alitumwa kwa mtaalamu wa picha za matibabu aliyetambuliwa kama Robert Kiplangat.

Katika chumba za picha, Bw Kiplangat alimshauri avue suruali na nguo zake za ndani.

Alitoka kwa muda mfupi katika chumba cha picha na muda mfupi alirudi na ndizi mbili akidai hospitali hiyo haikuwa na vifaa muhimu vya matibabu.

Inasemekana kwamba Bw Kiplangat alimwambia mgonjwa kwamba angeweka kondomu kwenye ndizi kama sehemu ya utaratibu huo.

Mwathiriwa aliwaambia polisi kwamba mhudumu huyo alimtaka alale kwenye kitanda akitazama ukuta.

Baadaye aliambia polisi kwamba alihisi uchungu kwa njia isiyo ya kawaida na alipogeuka, alipata Bw Kiplangat alikuwa amevua nguo, akiwa amevalia kondomu na kumwingilia.

Mwathiriwa alipiga kelele kuomba msaada lakini mlango ulikuwa umefungwa kutoka ndani. Bw Kiplangat alimuonya kutopaza sauti lakini mayowe yake tayari yalikuwa yamevutia wagonjwa wengine na wasimamizi wa hospitali.

Baadaye iliibuka kuwa Bw Kiplangat alikuwa amebadilisha picha iliyoagizwa na daktari kufanya uchunguzi wa uke wa mgonjwa.

Mwathiriwa aliripoti malalamishi hayo katika Kituo cha Polisi cha Ruiru na akafanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Ruiru Level 4.

Bw Kiplangat alikamatwa na baadaye alifikishwa katika Mahakama ya Ruiru mnamo Novemba 19.

Alikanusha mashtaka ya unyanyasaji wa kijinsia na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu ya Sh200,00. Lakini anadaiwa kwani hakuweza kupata dhamana na akazuiliwa rumande.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA