Gachagua: Msidhani Ruto amefuta Adani kwa hiari, alijua vizuri ilikuwa na ufisadi ila alinyamaza
NAIBU Rais wa pili wa Kenya Rigathi Gachagua amesema kwamba hatimaye ataondolewa lawama zote alizolimbikiziwa alipoondolewa mamlakani.
Bw Gachagua amesema kuwa moja ya madai ya kuondolewa kwake madarakani ilikuwa ni kuhujumu serikali kwa kumwambia Rais William Ruto ukweli kuhusu dili za Adani na ambao hatimaye umetimia.
“Nilikuwa mtu pekee ambaye ningethubutu kusema ukweli kwa rais. Shida yangu pekee na rais ilikuwa kusema ukweli. Kabla ya kuondolewa mamlakani, nilimwambia Rais Ruto kwamba mpango wa Adani haukuwa mzuri kwa nchi. Kulikuwa na ufisadi mwingi katika mpango huo. Majibu kutoka kwa rais yalikuwa ni kufanikisha kuondolewa kwangu kwa madai kwamba nilikuwa nikihujumu serikali yake, lakini baada ya muda, nitaondolewa lawama zote,” alisema.
Bw Gachagua alikuwa akizungumza katika kanisa la AIPCA Kangari katika Eneo Bunge la Kigumo, Kaunti ya Murang’a wakati wa ibada.
Naibu Rais huyo wa zamani alisema kuwa serikali imeziba masikio kwa vilio vya watu waliowachagua na kama si serikali ya Amerika kuingilia kati, mikataba ya Adani ingetekelezwa.
“Imechukua mkono wa serikali ya Amerika kwa Rais Ruto kubadilisha moyo. Haikuwa mapenzi yake bali nguvu za nje. Kwa nini tumefika hapa? Watu walikuwa tayari wamelalamika kuhusu mpango huo lakini serikali ilibaki kimya,” aliongeza.
Sasa Bw Gachagua anamtaka rais na viongozi wote waliochaguliwa kuwasikiliza wananchi kwa sababu wao ndio wakuu kuliko nyadhifa zao.
“Nawaomba viongozi wote waliochaguliwa wakiongozwa na Rais Ruto wawasikilize wananchi kabla ya kuwawekea sera za kuwafyonza. Tulifanya kampeni na kauli mbiu ya Mama Mboga lakini hakuna anayewazungumzia siku hizi, wasikilizeni wananchi. Ni wao waliowapa kazi hizo,” aliendelea.
Kuhusu kujitolea kwake katika kuhakikisha kuwa eneo la Mlima Kenya linasalia limeungana siku zijazo, alisema kuwa atatoa mwelekeo kuanzia Januari kuhusu safari ya kisiasa ya Mlima huo.
“Ninazungumza na viongozi mbalimbali, wa sasa na wa zamani, wataalamu, viongozi wa Kanisa na watu wengine na nitatoa mwelekeo hivi karibuni. Tayari tumewajua marafiki zetu na hata tutakuwa na wengi zaidi,” aliahidi.
Bw Gachagua aliandamana na viongozi wengi akiwemo Mbunge wa eneo hilo Joseph Munyoro, Seneta John Methu (Nyandarua), Kamau Murango (Kirinyaga), Joe Nyutu (Murang’a), Karungo Wa Thagwa (Kiambu) wabunge James Gakuya (Embakasi Kaskazini) Benjamin Gathiru Mejja Donk (Embakasi Kati) Amos Mwago (Starehe ) Edward Muriu (Gatanga).
Waliokuwa wabunge Ngunjiri Wambugu, (Mji wa Nyeri), George Theuri, (Embakasi Magharibi), madiwani wa kaunti hiyo wakiongozwa na MCA wa Wadi ya Kangari Moses Mirara miongoni mwa viongozi wengine.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA