Polisi wa utawala alivyonaswa katika genge linalopiga bei risasi, sare za vikosi vya usalama
MAAFISA wa polisi wamemkamata afisa wa polisi wa Utawala miongoni mwa washukiwa wengine waliokamatwa katika operesheni iliyofanywa mwishoni mwa wiki kufuatia uuzaji wa risasi.
Katika msako huo, polisi walifanikiwa kupata sare kadhaa za polisi na risasi zilizoibwa kutoka eneo la Rachuonyo Kusini mwishoni mwa juma. Mshukiwa huyo, Bw Robin Ochieng, anayehudumu Konoin, kaunti ya Bomet alikamatwa Jumapili baada ya washukiwa wengine wawili kunaswa walipokuwa wakijaribu kuuza sare za polisi.
Polisi walikuwa wameendesha operesheni iliyopelekea kupatikana kwa risasi na bidhaa zingine kutoka kwa nyumba ya afisa huyo.
Kisa hicho kilianza wakati Kamati ya Nyumba Kumi katika mji wa Oyugis walipokutana na wanaume wawili waliokuwa wakijaribu kuuza sare za polisi.
Baadaye wadokezi hao wa polisi waliwapasha habari maafisa wa usalama kuhusu biashara hiyo haramu. Mmoja wa washukiwa hao alikuwa Jeff Omondi, 18.
Alikuwa na risasi mbili aina ya milimita 7.62 na milimita 51, kofia na suruali moja ya polisi. Mshukiwa mwingine alikuwa Nashon Odwar, 19. Alikuwa na koti moja la polisi wa utawala na risasi mbili za milimita 7.62 x51.
Mshukiwa wa pili alifanikiwa kutoroka wakati wadokezi hao walipoamua kuwahoji ili kufichua walikopata silaha hizo.
Hata hivyo, alikamatwa na wapelelezi waliomtafuta na kumpata akiwa nyumbani kwa wazazi wake.
Katika ripoti ya polisi, mshukiwa wa kwanza alifichua kuwa walipewa silaha hizo na mwanamume mwingine aliyetambulika kama Samwel Otieno, 18.
Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Kusini, Philemon Saera alisema wanamzuilia mshukiwa wa tatu.
IMETAFSIRIWA NA SAMMY KIMATU