Wakenya washabikia nyuso mpya za uongozi wanazosema zinajali raia; watakuwa tofauti?
KUJITOSA kwa watu wapya katika kinyang’anyiro kijacho cha urais kumeibua gumzo jipya wakati huu ambapo raia wengine wanaonekana kupoteza matumaini yao kwa wanasiasa wa miaka mingi.
Wengi wamepoteza imani kwa utawala wa Rais William Ruto kutokana na sera zake zinazokandamiza watu wenye mapato ya chini na kadri.
Muungano mkuu wa upinzani, Azimio la Umoja-One Kenya nao unaonekana kusambaratika na kupoteza mwelekeo baada ya kinara wake Raila Odinga ‘kujiunga’ na serikali ya Dkt Ruto.
Ndiposa Seneta wa Busia Okiya Omtatah Okoiti na aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’a na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya wameibua msisimko na hisia mseto miongoni mwa Wakenya wa matabaka mbalimbali kwa kuashiria watawania urais 2027.
Kiongozi mwingine ambaye amewahi kutajwa kwa wadhifa huo kutokana na maadili na uzoefu wake ni aliyekuwa gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana.
Masuala ya kikatiba
Mtaalamu huyo wa masuala ya kikatiba hajatangaza iwapo ana azma ya kugombea urais japo amekuwa akionekana na aliyekuwa waziri Mukisa Kituyi na kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua wakikosoa serikali inapokiuka utawala wa sheria.
Sababu za kutajwa kwa Matiang’i, Omtatah na Natembeya ni misimamo yao mikali mbali na kwamba hawajawahi kupakwa ‘tope’ la siasa mbaya za Kenya wala kuhusika hasa katika sakata za ufisadi.
Jumamosi wiki iliyopita, Seneta Omtatah aliwashangaza Wakenya wengi alipotangaza kuwa amebuni kamati maalum ya kuendesha utafiti kuhusu ufaafu wake kama mgombeaji urais 2027.
Aidha, alisema kamati hiyo, ya wanachama 10, itakusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu changamoto muhimu za kitaifa na kupendekeza namna ya kushughulikia masuala hayo kupitia uongozi mkomavu na mbunifu.
Bw Omtatah alichapisha kwenye toleo la gazeti rasmi la serikali majina ya wanachama wa kamati hiyo itakayohudumu kwa miezi 18, hili likiwa wazo geni zaidi katika ulingo wa siasa nchini.
“Kibarua kijacho kinahitaji maandalizi bora, na awamu hii ya utafiti ni muhimu katika kuhakikisha kuwa maono yetu yanaoana na matumaini na ndoto za Wakenya,” akasema Ijumaa wiki jana.
Omtatah alijizolea sifa kwa kutetea wanyonge
Bw Omtatah, 60, alijizolea sifa kwa miaka mingi kama mtetezi wa haki na maslahi ya wanyonge kupitia kesi ambazo amekuwa akiwasilisha mahakamani kupinga sera, sheria na maamuzi mabaya ya serikali hii na zilizopita.
Baadhi ya kesi hizo ni zile za kupinga kuanzishwa kwa ushuru mpya, ubinafsishaji wa mashirika na mali ya umma na masuala ya kikatiba kama kupinga uhalali wa matokeo ya uchaguzi wa urais 2022.
Ni harakati kama hizo zilizomfanya kuhusudiwa na wananchi kiasi cha kushinda useneta wa Busia kwa tiketi ya chama kisicho na umaarufu cha National Reconstruction Alliance (NRA) katika ngome ya ODM.
Mnamo Juni mwaka huu, Omtatah alipokelewa kwa furaha na vijana wa Gen-Z katika bustani ya Uhuru, Nairobi walikokokangamana kuwakumbuka wenzao waliouawa kwenye maandamano, wakimwona mwenzao kama kielelezo cha vita dhidi ya utawala mbaya.
Huku Omtatah akitangaza azma yake, Dkt Matiang’i, ambaye anaishi Amerika, alitangaza nia ya kuwania kiti hicho na kuibua hisia mseto kutoka kwa umma.
Habari zilichipuza kwamba waziri huyo wa zamani aliyehudumu chini ya utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta, amekodi shirika la Dickens and Madson kuongoza maandalizi na kampeni zake za urais.
Kulingana na habari kwenye tovuti ya The Africa Report, Dkt Matiang’i mnamo Julai 13, 2024 alitia saini mkataba wa Sh32.5 milioni na shirika hilo la Canada.
Matiang’i ‘alichapa kazi nzuri’
Matiang’i alichapa kazi nzuri alipohudumu kama Waziri wa ICT na Elimu.Kati ya 2015 na 2018, alitekeleza mageuzi makubwa katika usimamizi wa mitihani ya kitaifa, hatua iliyopunguza pakubwa visa vya udanganyifu.
Na wakati wa maandamano wa Gen-Z, Matiang’i alipigiwa upato kama kingozi “bora” aliyepaswa kuchukua nafasi ya Rais Ruto kama Rais wa Kenya.
Hii ndiyo maana wale wanaounga mkono ndoto yake ya urais, wanamsawiri kama atakayerejesha maadili katika usimamizi wa asasi za umma.
Naye Gavana Natembeya ameweka wazi kuwa atawania urais “baada ya kukamilisha kibarua cha kuwahudumia watu wangu wa Trans Nzoia”.
“Kila kitu kinawezekana katika siasa. Kwa hivyo, kwa upande wangu baada ya kukamilisha kibarua ambacho watu wa Trans Nzoia walinipa nitawania urais. Sitakuwa mgombea mwenza wa yeyote,” akasema kwenye video.
Kwenye video hiyo Bw Natembeya hajabainisha ikiwa atawania urais 2027 au 2032.Lakini duru zinasema kuwa mipango inasukwa ili kumwezesha gavana huyo kuwa mgombeaji wa urais wa atakayeungwa mkono na wakazi wa Mlima Kenya.
Ni mapema kubashiri wa kumng’oa Ruto
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anasema bado ni mapema kubashiri mwelekeo wa siasa nchini wakati kama huu “licha ya kutokea kuwa nyuso mpya katika kinyang’anyiro cha urais”.
Hata hivyo, anabashiri kuwa huenda Wakenya wakachagua mtu mgeni kabisa kuwa Rais mwaka wa 2027 baada ya kuchoshwa na wanasiasa walioko sasa ambao wamewazoea tangu miaka ya 1990.
“Endapo maasi yaliyodhihirishwa na vijana wa Gen-Z yanaweza kujitokeza tena wakati wa kinyang’anyiro cha urais 2027, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba taifa hili linaweza kupata kiongozi mpya kabisa,” anaeleza akiongeza,
“Anaweza kuwa miongoni wa hawa wanaojitokeza au mwingine atakayetokea baadaye.”
Jaji Mkuu wa zamani David Maraga pia amependekezwa na Gen-Z kuwania urais.