Wito kukabili dhuluma za kijinsia, hasa mauaji ya kinyama dhidi ya wanawake na wasichana
KENYA na ulimwengu kwa jumla unapoadhimisha Siku 16 dhidi ya Dhuluma za Kijinsia, wito umeendelea kutolewa kukabili visa vya mauaji ya wasichana na wanawake ambavyo vimeendelea kuongezeka nchini na kuibua hofu kuu.
Mnamo Oktoba, Idara ya Huduma za Polisi ilieleza kuwa jumla ya visa 97 vya mauaji ya wanawake vilikuwa vimeripotiwa katika muda wa miezi mitatu iliyopita na kuelezea haja ya kuelekeza juhudi kabambe kukabili visa hivyo.
Mashirika ya kijamii, yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na wanaharakati, wametoa wito kwa mauaji haya yanayotekelezwa kinyama kutangazwa kama janga kwa taifa.
Juma lililopita, Rais William Ruto aliahidi Sh100 milioni za kusaidia kupiga vita dhuluma za kijinsia na kukomesha mauaji dhidi ya wanawake.
Akizungumza Ikulu akiwa ameandamana na viongozi wa kike, Rais alieleza kuwa juhudi hizo zitashuhudiwa katika kipindi hiki kilichoanza Novemba 25 had Desemba 10, 2024 kukabili visa vya dhuluma za kijinsia.
Visa vilivyoshuhudiwa hivi punde ni miili ya wanawake waliouawa kwenye magunia na kutupwa kwenye jaa za taka huku wengine wakiangamia kutokana na mizozo ya kinyumbani.
Alieleza kuwa jamii inastahili kuhamasishwa kuhusu hatari zilizopo au jinsi ya kuzitambua, huku akielezea haja ya hasa vijana kuwa makini wanapotumia mitandao ya kijamii ili kuepuka mitego ya wahalifu au watu wenye nia mbaya.
Rais pia alihimiza vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa washukiwa wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Usawa (NGEC), imeelezea hofu yake kwamba tangu 2022 ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake limeshuhudiwa, mauaji yakionekena kutekelezwa kwa msingi wa jinsia yao. Pia inasikitika kuwa baadhi ya wanaotekeleza mauaji hayo, ni wapenzi, au watu wa familia na walio karibu na waathiriwa.
Kupitia taarifa yake, Kaimu mwenyekiti wa tume, Thomas Koyier, anapongeza hatua ya Rais ya kutenga fedha za kukabiliana na hali hiyo, huku ikipendekeza sekta ya kibinafsi na jamii kujumuishwa katika juhudi za kusaka suluhu dhidi ya dhuluma hizo, kuimarisha ulinzi wa kisheria, na kuzindua makazi salama na vituo ambapo waathiriwa wanaweza kukaa hii ikijumuisha watu wa jinsia zote katika kipindi cha kujituliza baada ya kushuhudia dhuluma.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), dhuluma dhidi ya wanawake hushuhudiwa katika kila taifa, na tamaduni na kuathiri mamilioni ya wanawake na wasichana.
“Athari na changamoto za kufikia usaidizi zinaongezeka hata zaidi kwa wanawake na wasichana wanaoishi katika hali za dharura. Kote ulimwenguni leo, mizozo mikali na ya muda mrefu imechangia ongezeko la kila aina ya dhuluma za kijinsia,” WHO inasema katika taarifa yake.
Siku 16 dhidi ya ghasia za kijinsia, ni kipindi cha kutoa wito wa kukomesha dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana. Siku hii huanza Novemba 25, ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Dhuluma dhidi ya Wanawake, hadi Desemba 10 ambayo ni Siku ya Haki za Kibinadamu.