Habari za Kaunti

Wakazi 1,000 wa visiwa vya Manda waambia korti wamepokonywa ardhi ikauziwa raia wa kigeni

Na RICHARD MUNGUTI November 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ZAIDI ya wakazi 1,000 wa Visiwa vya Manda Kaunti ya Lamu wamewasilisha kesi katika Mahakama kuu Nairobi wakiomba warudishiwe mashamba yao wanayodai yamenyakuliwa na mabwanyenye wakisaidiwa na maafisa katika wizara ya ardhi na wakili.

Kupitia kwa Bi Fatuma Mahmoud na Wafiya Hussein, wakazi hao wanadai haki zao kumiliki mali na ardhi zimekandamizwa na kunyanyaswa na Msajili wa ardhi katika afisi ya eneo la Lamu.

Vile vile, wakazi hao wamelalama kwamba jitihada zao kushtaki wakili mmoja na msajili huyo wa ardhi zimegonga mwamba kwa vile wamepata maagizo kisiri kutoka Mahakama Kuu ya Milimani Nairobi kuwazima maafisa wa kupambana na jinai kuwachunguza na kuwafungulia mashtaka.

Mahakama imeelezwa kwamba wakazi hao wamepigwa na butwaa kugudua kwamba ijapokuwa ni wao wako na hati miliki za mashamba yao, wizara ya ardhi imetoa vibali vingine vya umiliki wa mashamba yao kwa watu wengine ambao hawajawauzia ardhi yao.

Walalamishi hao wameeleza mahakama kuu Milimani kwamba “ni jambo la kustaajabisha wako na hati miliki ya mashamba yao lakini pia wizara ya ardhi imewapa watu wengine hati za mashamba yao.”

Wakazi hao wamesema mahakama kuu Malindi iliamuru mashamba yao ni yao na kamwe “hakuna mtu yeyote anapasa kudai umiliki kwa vile wao ndio wamiliki asili.”

Katika malalamishi kwa mahakama kuu kupitia mawakili Martina Swiga na Danstan Omari, wakazi hao wamedai wanyakuzi wa mashamba yao wamewasilisha kesi kisiri na kupata maagizo ya kuzuia maafisa wa DCI kuwachunguza.

Pia wamepata maagizo ya kuzuia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) asiwafungulie mashtaka kuhusiana na unyakuzi wa mashamba yao.

Wakazi hao wameomba mahakama kuu pia iwajumuishe katika kesi iliyoshtakiwa na Alex Githinji Njage kwa lengo la kuwasilisha ushahidi maridhawa kuwezesha mahakama kufikia uamuzi wenye busara.

Wakazi hao wameeleza mahakama kwamba wataipa mahakama kuu Nairobi ushahidi kamili kuhusu umiliki wa ardhi ya zaidi ekari 1,000 iliyo na thamani ya mabilioni ya pesa.

“Tunaomba hii mahakama kutushirikisha katika kesi iliyoshtakiwa na Bw Njage ili tuipe mahakama ushahidi wa asili ndipo itoe uamuzi wa haki na ulioshamiri ukweli mtupu,” Fatuma Mahmoud amedokeza katika ushahidi aliowasilisha mahakamani.

Kupitia kwa mawakili Swiga na Omari wakazi hao wamesikitika kupoteza ardhi yao kwa matapeli lakini wako na imani mahakama kuu Nairobi itarejesha ardhi yao.

Awali, wanasema Mahakama kuu Malindi ilikuwa imewatambua wakazi hao wa Manda kuwa wamiliki halisi wa mashamba yao lakini kukachipuka hatimiliki nyingine za wanyakuzi.

“Twaomba mahakama kuu iturehemu na kuturudishia ardhi yetu,” Mahmoud ameililia mahakama.

Wakazi hao wamefichua kwamba afisa mmoja wa usajili wa ardhi na wakili walishtakiwa kwa ulaghai wa ardhi lakini wakaachiliwa na mahakama ikidai DPP hakuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kesi dhidi ya watalaam hao wa masuala ya sheria.