Waziri: Tutaunda jopokazi kushughulikia uvamizi wa panya katika mashamba ya mpunga
SERIKALI inapanga kuunda jopokazi ili kutafuta jinsi panya wanaovamia mashamba ya mpunga katika mradi wa Mwea watadhibitiwa.
Waziri wa Maji, Unyunyuzaji na Usafi wa Mazingira, Eric Mugaa alisema kuwa panya ni tishio kubwa katika Mpango huo na tatizo hilo linafaa kushughulikiwa haraka.
Kulingana na Bw Mugaa, jopokazi hilo litajumuisha wanachama kutoka Wizara yake, Wizara ya Kilimo na wengine kutoka Kaunti ya Kirinyaga.
“Kasi ambayo panya hao wanaongezeka katika shamba na kuharibu mpunga inatia wasiwasi. Panya wanaathiri uzalishaji wa mpunga na mitego haitasaidia, lazima tafute suluhu la kudumu la tatizo hili,” alisema Bw Mugaa alipokuwa akizuru mradi huo Jumatatu.
Alisema serikali pamoja na viongozi wa eneo hilo wanataka wakulima kupata manufaa makubwa kutokana na kilimo cha mpunga na hivyo kuna haja ya kutafuta njia mwafaka za kuwadhibiti panya hao.
Wakulima walilalamika kuwa panya wanaharibu mazao yao na imekuwa vigumu kwao kuwamaliza panya hao.
“Tuna wasiwasi na uvamizi wa panya, tunahitaji usaidizi ili kuwaangamiza,” mmoja wa wakulima hao, Bw Simon Njogu alisema.
Wakulima hao walilalamika kwamba hata mitego iliyowekwa kwenye mashamba haisaidii.
“Panya ni wengi na hawawezi kudhibitiwa ipasavyo kwa kutumia mitego,” alisema Bw Njogu.
Wakulima hao walisema ni serikali ya kitaifa na kaunti pekee ndizo zinaweza kukabiliana na tishio la panya.
“Ni jukumu la serikali kuu na kaunti kuhakikisha kuwa zao letu la mpunga ni salama kwa usalama wa chakula,” mkulima mwingine alisema.
“Kamati ambayo inaongozwa na Seneta Kamau Murango iliniita kwa lengo la kutaka kujua tunachofanya kuhusu uvamizi wa panya,” akasema waziri.
Kuhusu konokono, Bw Mugaa alisema wanaweza kudhibitiwa kibayolojia.
“Konokono pia ni changamoto katika mradi huu na tunataka kujua kama samaki aina ya kambare wanaweza kuletwa ili kutumia kama lishe,” alisema.
Bw Mugaa alisema wakulima wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa mpunga na wanapaswa kusaidiwa. Mradi huo, mkubwa zaidi nchini Kenya unachangia asilimia 80 ya mchele unaotumiwa kitaifa.
Hivi majuzi, serikali iliagiza bwawa la Thiba katika kijiji cha Rukenya eneo bunge la Gichugu kupanua kilimo cha mpunga.
IMETAFSIRIWA NA SAMMY KIMATU