Tumempanga Raila vizuri hatahangaika kwenye kampeni za AUC – Mudavadi
MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi ameelezea kuwa kampeni za Raila Odinga kuhusu uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) zinaendelea barabara huku Waziri Mkuu wa zamani akisaka uungwaji mkono katika mataifa ya Afrika Magharibi.
Akiongea na wanahabari jana kuhusu historia ya miaka 60 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Kenya na mataifa ya nje, Bw Mudavadi, alielezea kuwa kampeni za Odinga zinapewa uzito mkubwa na Serikali ya Kenya.
“Kenya haijawahi kuongoza tume hiyo na huu ndio wakati na nafasi bora tuliyo nayo. Nilirejea nchini kutoka Angola jana (Jumatatu) ambako niliendesha kampeni miongoni mwa mataifa ya eneo la Maziwa Makuu.
“Rais William Ruto amewafikia marais wengi. Mimi pia nimezungumza na wengine wengi na tuna imani kwamba tutashinda uchaguzini jijini Addis Ababa mwaka ujao,” Bw Mudavadi akasema katika makao makuu ya wizara hiyo, Nairobi.
Aliandamana na Makatibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni, anayoiongoza; Dkt Korir Sing’oei na Roseline Njogu, miongoni mwa maafisa wengine wa wizara hiyo.
Wakenya ‘wajiepushe na propaganda’
“Nawaomba Wakenya wajiepushe na propaganda kuhusu namna kampeni hizi zinavyoendeshwa kwa sababu lengo letu ni kuunga mkono mmoja wetu na kuinua hadhi ya nchi yetu,” Bw Mudavadi akaongeza.
Aidha, alionya kuhusu mwenendo wa baadhi ya Wakenya “kurusha matusi kwa sababu hii ni shughuli yenye uzito mkubwa.”
Jana, Bw Odinga alifanya mkutano na Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, siku chache baada ya serikali kuendesha kampeni zake katika mataifa ya Afrika Kusini na Eneo la Maziwa Makuu wiki jana.
“Asante Mheshimiwa Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal kwa mapokezi mazuri Dakar. Ilikuwa fahari kujadiliana nawe kuhusu ugombeaji wangu wa wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika na maono yangu kwa bara letu. Nilifurahishwa na mapendekezo yako kuhusu namna ya kujenga Afrika yenye umoja, amani na ufanisi,” Bw Odinga akasema.
Bw Odinga pia alitua nchini Cote d’Ivoire ambako alifanya mazungumzo na Rais Alassane Ouattara na sasa anaelekea Nigeria Abuja Nigeria kusaka kura ya Rais Bola Ahmed Tinubu.
Wagombeaji wengine wawili
Katika uchaguzi huo, utakaofanyika Februari 5, 2025, Bw Odinga akabiliwa na upinzani kutoka wagombeaji wengine wawili.
Wao ni; Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Madagascar Richard James Randriamandrato.
Hata hivyo, wadadisi wanasema Bw Odinga na Bw Youssouf ndio wanaopigiwa upatu kushinda kiti hicho kinachoshikiliwa sasa na Moussa Faki Mahamat kutoka Chad anayekamilisha muhula wake wa pili.
Kando na marais Faye (Senegal) na Ouattara (Cote d’Ivoire), Bw Odinga pia amefanya msururu wa mikutano na marais wengine wa mataifa ya Afrika Magharibi ndani wa kipindi cha wiki moja iliyopita.
Mnamo Jumatatu aliuza sera zake kwa Rais wa Gambia Adama Barrow.
“Nilipata nafasi ya kukutana na Muhammad Jallow, makamu wa rais wa Gambia aliyenipa mapokezi mazuri. Aidha, nilizungumza kwa njia ya simu na Rais Adaman Barrow aliyekuwa ziarani katika ukanda huo wa Afrika Magharibi.
Mabadiliko makubwa
“Tulijadili azma yangu na maono ambayo ninayo ya kutekeleza mabadiliko makubwa ya bara letu, endapo nitachaguliwa,” Bw Odinga akasema.
Jumapili, Waziri huyo Mkuu wa zamani alifanya mazungumzo na Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo jijini Accra, siku moja baada ya kufanya mkutano na Rais wa Togo Faure Gnassingbé jijini Lome Jumamosi kuuza ajenda yake.
Kwenye taarifa katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X, Bw Odinga alimpongeza Addo kwa “kunipokea vizuri katika awamu hii ya ziara yangu katika Afrika Magharibi.