Jamvi La Siasa

Wabunge wataka kuona ukarabati wa afisi uliofanywa na Gachagua, uliomeza Sh1.2 bilioni

Na SAMWEL OWINO November 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

WABUNGE wameshuku uhalali wa mabilioni ya fedha zilizotumiwa na Afisi ya Naibu Rais wakati wa hatamu ya Rigathi Gachagua kugharamia ukarabati wa afisi za jumba la Harambee Annex, makazi ya Karen na afisi ya Naibu Rais iliyoko Mombasa.

Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Usalama na Utawala sasa inataka maelezo kuhusu kazi zote za ukarabati zilizofanywa chini ya usimamizi wa afisi hiyo hadi mwishoni mwa mwaka wa kifedha wa 2023/2024.

Kuashiria kuwa wanashuku matumizi ya kiasi hicho kikubwa cha fedha katika shughuli hizo, wanachama wa kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo, wanataka kuzuru sehemu hizo tatu kuthibitisha ikiwa kazi iliyofanywa inaafiki pesa zilizodaiwa kutumika.

Stakabadhi zilizowasilishwa mbele ya kamati hiyo Jumanne, Novemba 26, 2024 zinaonyesha kuwa kufikia Juni 30, 2024 afisi ya Naibu Rais ilikuwa imetumia Sh98.40 milioni kukarabati afisi ya Harambee Annex iliyoko katikati mwa jiji la Nairobi.

Afisi ya Mombasa

Aidha, zilionyesha kuwa Sh249 milioni zilitumika kukarabati Makazi Rais ya Naibu Rais katika mtaa wa Karen huku Sh49 milioni zikitumiwa kukarabati afisi ya Mombasa ambayo Bw Gachagua alikuwa akitumia akiwa ziarani Pwani.

Kamati hiyo pia inataka maelezo kuhusu namna Sh771.7 milioni zilizotengewa Afisi ya Mkewe Bw Gachagua Dorcas Rigathi zilitumika katika mwaka huo wa kifedha wa 2023/2024.

Kamati hiyo pia ilichambua ripoti kuhusu utekelezaji wa bajeti katika Afisi ya Naibu katika kipindi cha miezi sita ya mwisho ya mwaka huo wa kifedha.

Katika kipindi hicho, stakabadhi zilizowasilishwa mbele ya kamati hiyo zinaonyesha kuwa Afisi ya Naibu Rais ilitengewa Sh100.4 milioni za kukarabati Afisi ya jumba la Harambee Annex, Sh250 milioni za kukarabati makazi ya Karen na Sh50 milioni kufadhili ukarabati wa afisi ya Mombasa.

Kwa misingi hiyo, gharama ya ukarabati wote wa Afisi ya Naibu Rais iliyoko jumba la Harambee Annex ni Sh450.4 milioni, gharama ya ukarabati wa makazi ya Karen nayo ilifyonza Sh560 milioni huku pesa zote zilizotumika kugharamia ukarabati wa afisi ya Mombasa zikiwa Sh240 milioni.

Ilitarajiwa kukamilishwa Juni 2027

Inakadiriwa kuwa miradi hiyo yote ilitarajiwa kukamilishwa kufikia Juni 2027.

Maafisa kutoka Afisi ya Naibu Rais waliwaambia wabunge wanachama wa kamati ya usalama kwamba baadhi ya kazi zilizofanywa katika makazi ya Kareni ni kupanuliwa kwa vyumba vya mikutano katika orofa za tatu na nne kwani ni vidogo.

Kazi zingine zilikuwa upanuzi wa jikoni saba, kupaka rangi, kuweka mataa mapya katika jengo hilo lote na kuboresha kamera za usalama (CCTV) zilizoko katika jengo hilo.

Wakati wa mkutano na maafisa wa afisi ya Naibu Rais wakiongozwa na Katibu Mku Msimamizi (PAS) Moses Mbaruku, wanachama wa kamati hiyo pia walishuku kiwango cha kazi ambacho kimefanywa kufikia sasa katika makazi ya Karen na afisi mbili za Nairobi na Mombasa, ikilinganishwa na pesa ambazo tayari zimetumika.

Stakabadhi zinaonyesha kuwa kufikia Juni 2024, ni asilimia 22 pekee ya kazi ya ukarabati imefanywa katika Afisi ya Harambee Annex, asilimia 45 katika makazi ya Karen ilhali asilimia ni asilimia 21 pekee ya kazi imefanywa katika Afisi ya Mombasa.

“Tunahitaji maelezo kamili hatua ambayo imepigwa kufikia sasa katika ukarabati wa afisi ya Harambee Annex, afisi ya Mombasa na makazi ya Karen,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Tongoyo.

Mbunge wa Narok Magharibi

Mbunge huyo wa Narok Magharibi alisema kiwango cha kazi kilichofanywa katika afisi ya Mombasa kufikia sasa hakilandani na kiwango kilichoonyeshwa kwenye stakabadhi zilizowasilishwa mbele ya kamati hiyo.

Aidha, Bw Tongoyo alifichukuwa kamati yake imepata habari kuwa kazi za ukarabati katika makazi ya Karen zimekamilishwa.

“Duru zingine zinatuarifu kuwa kazi iliyoratibiwa imekamilishwa na jengo lote la makazi Karen linatumika kikamilifu,” akaeleza.

Bw Tongoyo alihoji ni kwa nini makazi ya Karen ambayo ujenzi wake uligharimu Sh600 miliooni sasa inahitaji Sh560 milioni kufanyiwa ukarabati.

“Tunaambiwa kuwa jengo hilo la makazi ya Naibu Rais lilijengwa kwa gharama ya Sh600 milioni, kiasi cha pesa kinachokaribia zile zinazohitaji kuifanyia ukarabati,” Bw Tongoyo akasema.

 Naibu mwenyekiti wa Kamati hiyo Dido Rasso pia alihoji mantiki ya matumizi ya hadi Sh500 milioni kwa ukarabati pekee.

‘Sh500 milioni zilizotumika sio kidogo’

“Shilingi 500 milioni zilizotumika katika ukarabati sio kidogo. Je, una hakika kwamba wanachama wa kamati hii wakizuru maeneo hayo, tutapata kuwa pesa hizo zilitumika kweli na thamani yake ilipatikana” akauliza Bw Rasso ambaye ni Mbunge wa Saku (UDA).

Kamati hiyo pia ilihoji kuhusu matumizi ya  Sh5,023, 000 ambazo Afisi ya Naibu Rais ilipata kutokana na uuzaji wa vitu vikuu kuu.

Ingawa Paul Kimani, afis kutoka Afisi ya Naibu Rais alisema kuwa pesa hizo zilitumika kwa idhini ya Hazina ya Kitaifa, wabunge walisema hakukuwa na barua yote ya kuonyesha hilo na pesa hizo hazijarekodiwa miongoni mwa zile zilizopokewa na Hazina Kuu.

“Tulipata idhini kutoka kwa Hazina ya Kitaifa kutumia pesa hizo na kunayo barua ya kuthibitisha hilo,” Bw Kimani akaiambia kamati hiyo.

Hata hivyo, kamati hiyo ilisema kuwa Afisi ya Naibu Rais ingepewa mgao wa bajeti uliopunguzwa kwa kima cha Sh5 milioni katika mwaka huo wa kifedha ikiwa waliruhusiwa kutumia pesa hizo bila ya kuzituma kwa Hazina ya Kitaifa.

“Sio pesa nyingi, lakini ni pesa za umma. Mrejee afisini na muiandikie kamati hii barua mkielezea kuhusu zilizoko pesa hizo,” Bw Tongoyo akasema.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA