Lugha, Fasihi na Elimu

Matatizo yanayotokana na maneno ya mkopo: ni ghorofa, gorofa, horofa au orofa?

Na IRIBE MWANGI November 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JUMAMOSI ya tarehe 16.11.2024, jengo la ghorofa nne lilianguka mtaani Kariakoo jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Shughuli za uokozi ziliendelea kwa siku kumi ambapo watu 29 walitangazwa kufariki. Hili ni jambo la kuhuzunisha na tunaomboleza na ndugu zetu Watanzania.

Wakati wa kuomboleza, kulizuka mjadala mkali mtandaoni kuhusu matumizi ya maneno ghorofa, gorofa, horofa na orofa. Asili ya neno ilikubalika na wote kuwa neno ghurfah la Kiarabu.

Kutokana na mtagusano wa lugha na kuwepo kwa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kuigwa kwa utamaduni mgeni, lugha hukopa maneno kutoka kwa lugha zingine.

Maneno yanapokopwa, huwakilisha dhana fulani ambayo mara nyingi huwa ni geni kwa lugha inayokopa. Maneno hayo hubadilishwa na kuchukuwa muundo wa kitahajia wa lugha pokezi.

Hili huyafanya maneno kutamkika kwa urahisi na wapokezi. Hutokea hasa pale lugha inayopokea inapokosa baadhi ya sauti zilizo kwenye neno linalokopwa au pale ambapo mifumo ya matamshi na mpangilio wa sauti ni tofauti.

Katika Kiarabu, neno ghurfah lina maana “chumba” lakini linapokopwa katika Kiswahili, dhana ya jengo refu lenye zaidi ya sakafu moja inaingia.

Kuna wasomi waliosema kwamba ghorofa ni jengo lenyewe katika ujumla na pia sakafu tofauti kwa maana, “Hili ghorofa ni lake” na “Jumba hili lina ghorofa nne” ilhali baadhi walieleza kwamba jengo lenyewe ndilo ghorofa ilhali sakafu tofauti ni orofa kwa maana ya “Ghorofa la orofa nne.” Wengine walitumia maneno gorofa na horofa.

Kuna umuhimu wa kusanifisha maandishi na matumizi ya maneno kama haya.