Yafichuka asilimia 10 ya wanaume Kenya hudhulumiwa na wake zao
DHULUMA za kijinsia (GBV) dhidi ya wanawake na wasichana zinaendelea kuchangia ukiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani, Naibu Mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake nchini (UN) Done Basila, amesema.
Bw Basila alisema kuwa nchini Kenya takwimu zinatoa taswira mbaya ambapo asilimia 10 ya wanaume wamefanyiwa unyanyasaji wa kimwili katika kipindi cha miezi 12 huku akiongeza kuwa asilimia 34 ya wanawake na asilimia 27 ya wanaume wamedhulumiwa tangu wakiwa na umri wa miaka 15. Asilimia 16 ya wanawake wamenyanyaswa katika kipindi hicho.
Hivyo basi, alitoa wito kwa wadau wote kushiriki kikamili kampeni ya Kenya ya kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
“Lazima tukabiliane na ukweli kuhusu unyanyasaji wa wanawake na wasichana ambao ni moja ya ukiukaji mbaya zaidi wa haki za binadamu duniani.”
“Kulingana na takwimu kutoka Utafiti wa Hali ya Familia Kenya Demographic 2022, asilimia 16 ya wanawake na asilimia 10 ya wanaume wamedhulumiwa kimwili katika muda wa miezi 12 iliyopita,” alisema Basila akiwa katika Uwanja wa Michezo wa Unoa mjini wa Wote wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga vita unyanyasaji wa jinsia.
Alisisitiza haja ya serikali na sekta ya kibinafsi kuchukua hatua za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake.
“Hii ni pamoja na kutekeleza mikakati ya kina kwa ushirikiano na mashirika ya kutetea haki za wanawake na kutenga bajeti muhimu,” alisema.
“Pia kuripoti kikamilifu maendeleo ya kukomesha hali ya kutojali na kuzuia unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kwa haraka hasa mauaji ya wanawake ambayo yameongezeka,” Basila alisema.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa siku 16 za uanaharakati ni muhimu katika kukumbusha jamii wajibu wa kupinga kanuni zinazodhuru na kuwekeza katika mabadiliko.
Aidha alisema kukomesha unyanyasji wa jinsia si jukumu la sekta moja, mtu binafsi au shirika bali inahitaji jamii nzima kujitolea kwa usawa wa kijinsia.
Huku akisema serikali imeweka mifumo ya kisheria kama vile Sheria ya Ulinzi dhidi ya Dhuluma Nyumbani, Sheria ya Makosa ya Kingono na Sera za Kusaidia Waathiriwa, utafiti unaonyesha kuwa wanawake na wasichana bado wanapitia unyanyasaji wa kimwili na kingono.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Wanawake wa Makueni Rose Museo, alilaumu unywaji pombe na utumizi wa dawa za kulevya akisema ni chanzo kikuu cha Unyanyasaji wa Kijinsia katika kaunti hiyo.
Museo alitoa wito kwa serikali kupambana na tabia hiyo ili kuhakikisha inakabiliana na matumizi ya dawa za kulevya katika jitihada za kukomesha unyanyasaji wa jinsia.
Aidha, aliwataka wanawake walio katika ndoa kuepuka kusababisha migogoro katika familia zao ili kuepuka unyanyasaji ambao umekithiri katika eneo hilo.
“Ninaiomba serikali ya kitaifa kuhakikisha unywaji wa pombe na matumizi ya dawa za kulevya unakomeshwa ili kuepusha migogoro katika familia,” alisema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA