Habari Mseto

Shosho wa miaka 90 aomba korti iamuru arejeshewe shamba lililotwaliwa na serikali 1973

Na RICHARD MUNGUTI November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NYANYA mwenye umri wa miaka 90 Jumatano (Novemba 27 2024) aliiomba Mahakama kuu iwarudishie shamba lao la ukubwa wa ekari 818 lenye thamani ya zaidi ya Sh3 bilioni iliyotwaliwa kimakosa na serikali miaka 54 iliyopita.

Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Anne Omollo, Bi Miriam Wahu Kagiri aliyesaidiwa na bintiye kuingia kizimbani alifichua alikuwa na umri wa miaka 34 aliponunua ekari nne za shamba hilo kwa bei ya Sh1,400 mwaka wa 1966.

Bi Kagiri alisema kwa kila ekari alikuwa analipa Sh350.

Alitoa risiti alizolipia shamba lake kama ushahidi.

Bi Kagiri alimweleza Jaji Omollo kwamba kabla ya kufurushwa kutoka kwa shamba hilo lililoko eneo la Kang’undo Road na maafisa wa polisi na Askari wa Baraza la Mji alikuwa amejenga nyumba za mabati na alikuwa analima.

“Kabla ya kufurushwa kutoka kwa shamba hilo na maafisa wa polisi na askari wa kanjo 1973 nilikuwa nimejenga nyumba za mabati,” Bi Kagiri alisema.

Aliongeza kusema kuwa alikuwa anakuza mimea ya chakula kama vile mahindi, maharagwe na mboga miongoni mwa vyakula vingine.

Nyanya huyo aliyetoa ushahidi kwa lugha ya Kikuyu na kutafsiriwa na karani wa mahakama Susan Nyambura alisema “hawakulipwa fidia baada ya kutimuliwa shambani mwao na serikali.”

Jaji Omollo alielezwa na Bi Kagiri kwamba shamba hilo lilimilikiwa na Khan Family.

Wakiwa wanachama 225 wa kampuni ya Kiambu Dandora Farmers Company Limited (KDFCL) walinunua shamba hilo kwa bei ya Sh286,300 kati ya 1966-1967.

“Ulizaliwa lini? Ulikuwa na umri wa miaka mingapi mkinunua shamba hilo,” Jaji Omollo alimuuliza Bi Kagiri.

Akajibu: “Nilizaliwa mwaka wa 1934. Tukinunua shamba hili nilikuwa na umri wa miaka 34. Na sasa niko na umri wa miaka 90. Nimezeeka na bado zijafurahia matunda ya jasho langu.”

Nyanya huyo alieleza jaji huyo kwamba ijapokuwa alipewa hati ya umiliki wa shamba hilo na afisa wa usorovea hajajenga vile alikuwa ananuia akinunua shamba hilo.

Mahakama ilielezwa shamba hilo liko kati ya Dandora Phase l na Kayole.

Nyanya huyo alisema ni matumaini yake shamba hilo warudishiwe kabla ya kuaga dunia angalau ajenge na kukaa katika nyumba ya kifahari aliyokusudia.

Jaji Omollo alielezwa na Katibu Mkuu wa KDFCL Karanja Mwangi kwamba shamba hilo lilitwaliwa na Serikali 1970 kwa ajili ya maslahi ya umma.

Lakini alisema “shamba hilo liliishia mikononi mwa watu binafsi ambao wameistawisha.”

Bw Mwangi alisema baadhi ya taasisi za umma zilizomo kwenye shamba hilo ni pamoja na Hospitali ya Mama Lucy Kibaki, Mtaa wa Umoja II na Afisi za Utawala wa Mikoa.

“Kati ya ekari 818 ni sehemu ya ekari 20 zilizopewa wanachama wa KDFCL. Nyingine zimenyakuliwa na watu binafsi,” alisema Bw Mwangi.

Katibu huyo alisema kampuni ya KDFCL ndiyo iliyo na hatimiliki ya shamba hilo ambalo linang’ang’aniwa pia na kampuni ya Dandora Housing Scheme Limited (DHSL).

Kampuni hizi mbIli KDFCL na DHSL zimepambana kufa kupona kila moja ikidai ndio mmiliki wa shamba hilo.

Kesi hii ya umiliki wa shamba hili ilisikizwa na majaji zaidi ya 40.

Bw Mwangi alimweleza Jaji Omollo kwamba KDFCL ilitangazwa mmiliki wa shamba hili na Jaji (marehemu) Kasanga Mulwa.

Nayo DHSL inasema kwamba ilitangazwa mmiliki halisi wa shamba hilo na Jaji Frank Shields aliyeamuru aliyekuwa msajili wa mahakama marehemy Bhatt arudishe wizara ya ardhi pesa ilizoweka kortini kama fidia baada ya kulitwaa shamba hilo.

Hata hivyo Bw Mwangi alisema KDFCL haikulipwa fidia na serikali akiongeza “mahakama ilikosoa serikali kwa kutwaa shamba hilo kinyume cha sheria.”

Bw Mwangi alisema serikali ilinyakua shamba la KDFCL kuwapa mabwanyenye.

Jaji Omollo aliahirisha kusikizwa kwa kesi hiyo hadi Juni 4 2025.