Habari Mseto

Mwanamke taabani kwa shtaka la kumtapeli mwanaume Sh447,000

Na RICHARD MUNGUTI, LABAAN SHABAAN November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SUSAN Gathoni Karuthi ameshtakiwa kwa kumlaghai mfanyakazi wa hoteli Sh447,000 akidai atamuuzia gari la kifahari.

Bi Gathoni aliyefikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Gilbert Shikwe alikana alimlaghai Delvis Muoki Mutua pesa hizo akijifanya alikuwa na uwezo wa kumuuzia gari.

Gathoni mwenye umri wa miaka 33 alikabiliwa na shtaka la kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu kinyume na sheria nambari 313 za uhalifu.

Upande wa mashtaka ulisema katika kipindi cha miezi tisa kati ya Desemba 7 2023 na Agosti 16 2024, katikati mwa jiji la Nairobi, Gathoni alipokea Sh447,000 kutoka kwa Bw Mutua akidai atamuuzia gari, jambo alilojua hawezi.

Kiongozi wa mashtaka Bi Judy Koech alimweleza hakimu baada ya Gathoni kupokea pesa hizo kutoka kwa Bw Mutua, alianza mchezo wa paka na panya hadi pale alipotiwa nguvuni Novemba 15, 2024 na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Central.

Susan Gathoni Karuthi akiwa kortini. Picha|Richard Munguti

Bi Koech alisema Gathoni hakumnunulia gari Bw Mutua kama alivyoahidi.

Bi Gathoni aliomba hakimu amwachilie kwa dhamana na kuahidi, “nitatii maagizo nitakayopewa na mahakama endapo itaniachilia huru kwa dhamana.”

Bi Koech hakupinga na mshtakiwa akaachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni.

Iwapo mshtakiwa atashindwa kulipa dhamana hiyo alimpa dhamana badala ya Sh200,000 pesa tasilimu.

Kesi itatajwa Desemba 4, 2024 kwa maagizo zaidi.