Habari Mseto

Wanafunzi kutoka familia maskini wafanyiwa sherehe kwa kukamilisha vyema KCSE

Na FRIDAH OKACHI November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANAFUNZI zaidi ya 20 kutoka familia maskini, mtaa wa Kawangware walifanya sherehe ya kufunzu kuashiria kukamilisha mtihani wa Kidato cha Nne baada ya kufadhiliwa miaka minne na Shirika la Every Girls Count (EGC).

Kulingana na Shirika hilo, lilijitolea kusaidia wanafunzi hao ambao walishindwa kujiunga shule na hivyo kuwalipia karo katika shule za kutwa.

Wanafunzi hao ambao walipata alama zaidi ya 350 katika mtihani wa darasa la nane, walipewa fursa ya kujiunga na shule za kutwa.

Esther Achieng ambaye alijawa na furaha kwa kuvalia gauni, alisema aliepuka kurejea kijijini kuungana na mamake mzazi baada ya mfadhili kumtafutia nafasi na kujiunga na shule kutwa ya Upili ya Dagoretti.

Mkurugenzi wa Shirika la Every Girl Counts Emmanuel Katana akiongeza na wanafunzi 20 kutoka shule za kutwa wakiwa wamevalia magauni baada ya mtihani wa Kidato cha Nne 2024, KCSE. Picha|Fridah Okachi

“Nafurahi kukamilisha masomo yangu bila tatizo kama wenzangu mtaani. Nilipopata barua ya kujiunga na Kidato cha Kwanza nje ya Nairobi, niliona ndoto yangu imetimia.  Wazazi walikuwa wameshindwa kulipa karo kwa sababu nilikuwa na ndugu wengine katika shule za upili na mmoja chuo kikuu,” alisema Achieng.

Aliongeza kuwa wazazi wake walishindwa kulipa karo hiyo, babake ambaye ni bawabu akitegemea mshahara wa Sh12,000 pekee kukimu maisha ya familia, naye mamake akisalia mashambani.

Kando na Achieng, Damaria Bocheni ambaye ni yatima alifahamu kuwa atarejeshwa mashambani na mjombaye pindi tu matokeo ya mtihani wa darasa la nane yalipotangazwa. Wasiwasi ulimjaa Bocheni kwa kuwa mjombaye alitegemea kibaru cha mjengo.

“Nilifululiza hadi katika afisi za kusaidia wasichana. Mlezi wangu ndiye alikuwa mama na baba kwa wanawe na pia kwangu. Alinifahamisha hana uwezo wa kunisomesha licha ya kupata alama zaidi ya 300,” alidokeza Bocheni.

Mkurugenzi wa Shirika la Every Girl Counts Bw Emmanuel Katana alisema walisherehekea wanafunzi hao ambao walipatwa na changamoto wakati mgumu wa Covid-19 (mwaka 2020-2021) na mafuriko wakiwa darasa la nane na pamoja na mafuriko katika mwaka 2024.

Mwazilishi wa Shirika la Every Girl Counts akizungumza katika sherehe ya kufunzu kwa wanafunzi hao wa Kidato cha Nne, KCSE. Picha|Fridah Okachi

“Naamini mtoto wa kike akipewa elimu, jamii inaimarika. Hapo mbeleni kulikuwa na shida ya kupelekwa shuleni. Hivi sasa, katika mtaa wa Kawangware mzazi akiwa na msichana na mvulana wanaofaa kujiunga na shule ya upili, iwapo ana uwezo wa kusomesha mtoto mmoja, mvulana atapewa kipaumbele,” alisema Bw Katana.

Mwazilishi wa shirika la EGC, Bi Renee Cook alisema mradi huo unalenga kutoa fedha za elimu kwa ajili ya kuwasomesha mtoto wa kike hadi shule ya upili wanaoishi katika mazingira magumu jijini Nairobi.

Bi Cook alisema kuwa japo elimu nchini Kenya ni tofauti na nchi ya Amerika, alitaka serikali kubadilisha mbinu na kuhakikisha kila mwanafunzi anajiunga na shule ya upili na kumaliza.

“Najua kunaweza kuwa na upungufu wa bajeti kwa serikali kutoa chakula cha mchana kwa mwanafunzi, na hapo ndipo tunapoingia kusaidia familia na kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula.”

Hadi kufikia sasa wanafunzi 80 kutoka mtaa huo wamepewa fursa ya kusoma katika shule ya upili, wanaofanya bora katika mtihani huo wa kitaifa wa kidato cha nne wakiendelea hadi chuo kikuu.