Aliyekuwa mbabe wa kivita Liberia aliyechochea mauaji ya Rais Samuel Doe afariki
MONROVIA, Liberia
ALIYEKUWA mbabe wa kivita nchini Liberia Prince Johnson, aliyechochea mauaji ya kinyama ya rais wa zamani Samuel Doe, amekufa akiwa na umri wa miaka 72.
Mauaji ya Doe yalipelekea Liberia kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 1989 na 2003 ambapo Johnson alihusika pakubwa.
“Ni kweli alikufa leo (Alhamisi) asubuhi,” Moses Ziah, mmoja wa watu wa familia yake aliambia shirika la habari la Reuters Alhamisi, Novemba 28, 2024.
Msemaji wa familia Wilfred Bangura pia alithibitisha kifo cha Johnson, ambaye alikuwa akiugua maradhi ya mikimbio ya damu.
Zaidi ya watu 200, 000 waliuawa na maelfu ya wengine kukatwakatwa na wengine kubakwa huku zaidi ya watu milioni moja wakipoteza makao katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Johnson alipata sifa mbaya baada ya wapiganaji wake kumkamata, kumtesa kabla ya kumuua kinyama rais Doe.
Katika video moja mnamo 1990, Johson alionekana akisherehekea huku wapiganaji wake wakikata masikio ya Doe kwa kisu kabla ya kumuua.
Baadaye, Johnson alisema alijutia mauaji hayo na kuomba maridhiano na familia ya Doe.
Licha ya kwamba Tume ya Haki na Maridhiano ya Liberia ilipendekeza ashtakiwe kwa uhalifu wa kivita, ikisema wapiganaji wake wakitekeleza ubakaji na mauaji, Johnson hakushtakiwa.
Baada ya vita hivyo, mbabe huyo wa kivita alisalia katika siasa na akachaguliwa kuwa Seneta katika ngome yake ya kaunti ya Nimba.
Baadaye alisaidia pakubwa wagombeaji urais katika chaguzi zilizofuata.
Kwa mfano, mnamo 2011 alimuunga mkono rais wa zamani Ellen Johnson-Sirleaf na akashinda na hivyo kuandikisha historia kama mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Liberia.
Vile vile, mnamo 2017 Johnson alimuunga mkono George Weah na akashinda urais dhidi ya Josephe Boakai aliyeungwa mkono na Sirleaf.