TAHARIRI: Maafisa waimarishe doria katika mipaka
NA MHARIRI
Huku Wakenya wakiendelea na mdahalo kuhusu jinsi magaidi wa Al-Shabaab walivyofanikiwa kujiandaa na kutekeleza mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi katika hoteli ya Dusit2D, 14 Riverside, mtaani Westlands, Nairobi, kuna kila sababu ya kuelekeza darubini katika maafisa wa serikali wanaohudumu maeneo ya mpakani.
Katika siku za hivi majuzi, raia wa kigeni wamenaswa nchini bila stakabadhi za usafiri.
Baadhi yao wamepatikana na vitambulisho na hati zingine za serikali ambazo walipata kwa njia ya ulaghai. Changamoto nyingi za kiusalama tunazokumbana nazo kwa sasa kama nchi zinatokana na kusambaratika kwa mfumo wa utawala wa kidemokrasia katika taifa jirani la Somalia. Kwa muda mrefu, nchi hiyo iliongozwa na magenge ambayo yalikamia kukumbatia uongozi wa kiimla chini ya msingi wa Sharia.
Baada kufurushwa kwa magenge hayo kutoka miji mikuu ya Somalia kama vile Mogadishu na Kisimayu, magaidi hao waliamua kusajili vijana wasio na kazi na wale walio na itikadi kali kutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara nchini.
Wito wetu ni kwa kila afisa anayehudumu katika sehemu za mpakani kuhakikisha wageni wanaoingia nchini wanachujwa kwa uangalifu mkubwa kabla kuruhusiwa kuingia nchini.
Ni usaliti ulioje, kwa mfano, kwa afisa wa uhamiaji katika eneo la mpakani kupokea kiasi kidogo cha pesa kisha kuruhusu wahalifu hatari ambao hatimaye hutekeleza mashambulizi kama lile la wiki jana katika 14 Riverside Drive?
Mbali na maafisa wa uhamiaji, kundi jingine ambalo linapasa kuimarisha doria ni polisi. Ripoti za awali za uchunguzi wa silaha zilizotumika na magaidi waliouawa zaonyesha kuwa, ziliagizwa kutoka Somalia.
Ni vipi magaidi hao waliweza kusafirisha zana hatari za kivita kama hizo umbali wa mamia ya kilomita kutoka sehemu ya mpakani hadi katikati mwa jiji bila kunaswa na makachero?
Hali ilivyo ni kwamba,maafisa wetu wa usalama watalazimika kubadilisha mbinu zao za kushika doria na kufanya ukaguzi wa magari katika vizuizi vya barabarani bila ilani ili kunasa magaidi kama hao kabla hawajamwaga damu kiholela nchini.
Utahisije kama afisa wa polisi kupokea hongo na kuruhusu magaidi hatari kuvuka mpaka kisha baadaye ukasikia wamevamia na kuangamiza na ndugu na jamaa zako?
Kimsingi, tunachosema hapa ni kwamba, ugaidi upo na kwa sasa ni jinamizi ambalo wengi wanajikuna kichwa kuhusu njia mwafaka zaidi za kukabiliana nalo. Hivyo basi, kila mmoja anapasa kuchangia kuhakikisha taifa letu ni salama kwetu sote.