Serikali ilituhadaa kutufidia, walia waathiriwa wa ghasia za 2007/8
Na CHARLES WASONGA
WAATHIRIWA wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu 2007 wameilaumu serikali kwa kutotekeleza ahadi yake ya kubuni Hazina Maalum ya kuwalipa ridhaa kwa mateso na hasara waliyopitia wakati wa machafuko hayo.
Mshirikishi wa kitaifa wa shirika la kutetea masilahi ya wahanga hao (National Victims and Survivors Network-NVSN) Wachira Waheire Jumatano alilalamika kuwa licha ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza mnamo 2015 kwamba hazina hiyo ingeundwa, afisi ya mwanasheria mkuu haijatoa mwongozo wowote wa kufanikisha ahadi hiyo.
‘Tangazo la Rais Uhuru Kenyatta bungeni mnamo 2015 kwamba hazina hiyo ingebuniwa mahsusi kwa ajili ya kuwalipa ridhaa mahasiriwa wa ghasia baada ya uchaguzi wa 2007 tuliingiwa na fuhara.
“Lakini tunasikishwa kuwa mpaka sasa hazina hiyo haijabuniwa kwa sababu ya uzembe wa maafisa fulani haswa Mkuu wa Sheria aliyeondoka Profesa Githu Muigai,” Bw Waheire akasema jijini Nairobi .
Alikuwa akihutubu katika kikao kilichoandaliwa na mashirika ya African Centre for Open Governance (AfriCog) na Kenya for Peace with Tuth and Justice (KPTJ) kujadili suala la haki kwa waathiriwa wa ghasia za kisiasa za 2007/2008.
Bw Waheire aliongeza kwamba mapema 2017 shirika hilo liliwasilisha ombi kuhusu suala hilo kwa afisi ya kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale lakini ombi hilo halijashughulikiwa mpaka sasa.
“Sasa mojawapo ya maazimio yetu katika mwaka huu mpya ni kufuatilia suala hilo kupitia Mkuu mpya wa Sheria Bw Paul Kihara kwa matumaini kwamba atalishughulikia suala hilo. Inasikitisha kuwa baadhi ya wahasiriwa wa ghasia za 2007 bado wanahangaika kwa kutolipwa fidia,” akalalamika.
Mshirikishi huyo wa waathiriwa alisema pesa ambazo serikali ya sasa iliwapa baadhi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani (IDPs) tangu 2013 pesa lakini “hazikutosha na zilitolewa kwa mapendeleo.”
“Hata majuzi nilipigiwa simu na mzee mmoja ambaye alipoteza mke na watoto katika Kanisa la Kiambaa mnamo 2008 ambaye mpaka sasa analalamika kuwa hajalipwa chochote. Hali ni hiyo hiyo kwa waathiriwa wengine walioko maeneo ya Nyandarua na Kisumu,” akasema Bw Waheire.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa AfriCog Gladwell Otieno aliitaka serikali kuanzia harakati za kubuniwa kwa Hazina hiyo maalum ili masuala yote ya ridhaa kwa waathiriwa yashughulikiwe kikamilifu.