Mnazurura bure, Ruto aambia wanaomezea mate urais
RAIS William Ruto amewapuuzilia mbali wapinzani wake wanaojiandaa kukabiliana naye katika uchaguzi wa urais wa 2027 akisema wanapoteza wakati wao bure.
Kwa majumaa kadhaa sasa, ulingo wa siasa umeanza kuchora taswira ya jinsi uchaguzi ujao wa urais utakuwa.
Akizungumza akiwa Taita Taveta hapo Jumatatu, Desemba 2, 2024, Dkt Ruto aliwataka wanaompinga wasubiri wakati mwafaka wa kampeni.
Kiongozi wa nchi alidokeza ana mpango wa makubaliano ya kisiasa ambao atafichua hivi karibuni.
“Kuna viongozi wengi wananishinikiza kuwajibu lakini nimewaomba watulie. Mashindano halisi yatakuwa 2027 na kwa sasa kila mmoja ajiandae,” akasema.
Narc Kenya kuondoka Azimio
Juma lililopita, Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua aliongoza wananchama wake kuondoka katika Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.
Alitumia chama hicho kuwania wadhifa kuwa mgombeaji mwenza katika uchaguzi mkuu wa 2022 pamoja na mwaniaji urais wakati huo Raila Odinga kwenye tikiti ya Azimio.
Kabla ya Bi Martha kuanza mchakato wa kuondoka Azimio, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alihudhuria hafla ambapo jamii ya Wakamba ilijumuishwa katika muungano wa Gikuyu, Embu na Meru (Gema).
Yapo mazungumzo yanayoashiria muungano kati ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Bw Musyoka.
Seneta wa Busia Okiya Omtatah pia ametangaza nia ya kuwania urais akilenga kuvuna kura za kizazi cha Gen Z ambacho kimeonekana kumpigia debe.
“Waache kuzurura na hadithi na hali hawana mpango madhubuti. Endapo wanaulizwa kwa nini wanapinga kitu ama waombwe kutoa mikakati yao, hawana chochote ila kuzurura tu. Lakini wacha nisiseme mengi, kuna mengi yanakuja na tutakutana wakati mwafaka,” akasema Rais Ruto.
Viongozi wanaopinga serikali
Rais aliandamana na mawaziri na wanasiasa mbalimbali.
Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed alipuuza viongozi na wanaharakati ambao wanapinga serikali.
Alijipiga kifua kuwa kiongozi wa upinzani ikizingatiwa kuwa yeye ni kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa.
Mnamo Agosti 2024, Bw Musyoka alijitangaza kuwa kiongozi rasmi wa upinzani baada kiongozi wa upinzani Bw Odinga kuzinduliwa rasmi kuwa mwaniaji wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
“Wale wote wanaozurura wakisema kuwa ni viongozi wa upinzani, wao ni feki. Wanafaa kuniacha nifanye kazi yangu,” akasema Bw Mohamed.
Rais na msafara wake walitua maeneo kadhaa katika Kaunti ya Taita Taveta kurai wakazi waunge mkono mpango wa afya wa Taifa Care na kusisitiza kuhusu umoja wa kitaifa.
Kulipia ada za kila mwezi
“NHIF ilikuwa na changamoto nyingi. Wakenya wachache tu waliweza kulipia ada ya kila mwezi. Usingoje hadi uwe mgonjwa ili ujisajili. Jisajili sasa katika mpango mpya ambapo Wakenya wote watapata matibabu wanapohitaji,” Rais alisifu bima mpya ya afya ambayo imekumbwa na changamoto na pingamizi.
Viongozi wengine ambao waliandamana na Dkt Ruto ni Gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime, Mwakilishi wa Kike Lydia Haika, na Wabunge John Bwire (Taveta), Danson Mwashako (Wundanyi), Peter Shake (Mwatate), na Abdi Chome (Voi).
Pia, walikuwepo Spika wa Seneti Amason Kingi na Mawaziri Opiyo Wandayi (Kawi), Hassan Joho (Madini) na Salim Mvurya (Biashara) wakiomba wananchi waunge mkono mipango ya Rais Ruto.