Makala

Yanayojiri katika kesi ya ununuzi wa kampuni ya Bamburi Cement, Bwanyenye akiachiliwa huru

Na RICHARD MUNGUTI, LABAAN SHABAAN December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 3

BWANYENYE Benson Sande Ndeta aliyeshtakiwa Ijumaa Novemba 29 kwa madai ya kuilaghai Benki ya Absa Sh4.5 bilioni, ameachiliwa bila masharti baada ya kutupwa rumande siku tatu katika kituo cha polisi cha Muthaiga.

Bw Ndeta aliachiliwa Jumatatu, Disemba 2 na hakimu mwandamizi Gilbert Shikwe baada ya mahakama kuu kupiga breki kushtakiwa kwake.

Wakili Cecil Miller alimkabidhi Bw Shikwe agizo kutoka Mahakama Kuu iliyositisha kukamatwa na kushtakiwa kwa Bw Ndeta.

“Jaji Bahati Mwamuye aliamuru Bw Ndeta asishtakiwe hadi kesi aliyowasilisha katika mahakama kuu isikizwe na kuamuliwa,” Bw Miller anayemwakilisha bwanyenye huyo pamoja na wakili Edgar Busiega aliambia mahakama.

Benson Sande Ndeta (kushoto) azungumza na wakili kizimbani. Picha|Richard Munguti

Wakili huyo alisema polisi hawakumwachilia mshtakiwa licha ya kufahamishwa kuhusu agizo la kuwazuia kumtia nguvuni.

Bw Miller alisema polisi walikwepa ili wasikabidhiwe agizo hilo hadi Jumatatu walipomfikisha kortini.

Akiwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana kwa Bw Ndeta, Bw Miller alisema kesi dhidi ya mwekezaji inatokana na ushindani wa kibiashara baada ya kununua kampuni ya saruji ya Bamburi Cement Limited kwa bei yaSh27.5bilioni.

Bw Miller alifichua kwamba Bw Ndeta kupitia kwa kampuni yake Savana Klinker ilishinda kampuni ya Tanzania ijulikanayo Amson katika ununuzi wa Bamburi Cement.

Mahakama ilielezwa kwamba ni jambo la kustaajabisha na kutamausha kuona asasi za kiusalama zikimfungulia mashtaka mwekezaji huyu ambaye ametoa ajira kwa maelfu ya Wakenya.
Pia mahakama ilielezwa mshtakiwa anadhulumiwa na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini.

Bw Ndeta alikana mashtaka tisa mbele ya Bw Shikwe.
Kiongozi wa mashtaka Judy Koech alipinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana akisema “atavuruga mashahidi kutokana na ushawishi mkubwa alionao.”

Mahakama ilielezwa kwamba makazi ya mshtakiwa hayajulikani na akiachiliwa atatoroka.

Bi Koech alisema polisi hawajapata pesa ambazo Benki ya Absa ililaghaiwa kati ya 2017 na 2018 na mshtakiwa.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na mawakili Cecil Miller na Busiega.

Waliambia mahakama mshtakiwa ni raia wa Kenya na mwekezaji katika sekta ya utengenezaji saruji.

Korti ilielezwa ikiwa kuna muwekezaji anayestahili kuungwa mkono na serikali basi ni Bw Ndeta.

Bw Miller aliambia mahakama kwamba ni maajabu kwamba Bw Ndeta ameshtakiwa kwa sababu ya kupewa mkopo wa benki kuwekeza katika biashara ya uzalishaji mali.

“Ni jambo la kustaajabisha na kutamausha kwamba Bw Ndeta ameshtakiwa kwa kukopa pesa kutoka kwa benki kuwekeza,” Bw Miller alimweleza hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bw Gilbert Shikwe.

Mahakama ilielezwa benki hutoa mikopo ya kibiashara kwa wawekezaji kustawisha biashara zao na kuzalisha bidhaa zaidi kwa lengo la kuongeza mtaji na mapato ya nchi.

Wakili huyo alieleza mahakama kwamba mwongozo wa serikali ni kuwahimiza wananchi kuwekeza katika viwanda vya kuzalisha mali ndipo ajira ipatikane.

Wabunge Paul Nzengu (kushoto) na Peter Salasyia (Mumias Mashariki) wazugumza baada ya kuachiliwa kes bwanyenye Benson Sande Ndeta katika kesi ya ulaghai wa Sh4.5 bilioni. Picha|Richard Munguti

Bw Miller alisema Bw Ndeta alikopeshwa pesa na Benki ya Absa kuwekeza katika biashara ya utengenezaji saruji na ikiwa ameshindwa kuuliza mkopo huo basi amana aliyoweka kupewa mkopo inafaa kuuzwa badala ya kushtakiwa.

“Ikiwa mwekezaji huyu alishindwa kulipa basi benki iko huru kutwaa mali iliyowekwa kama amana kuuzwa kwa njia ya mnada lakini sio kumfungulia mashtaka ya uhalifu,” Bw Miller alieleza mahakama kwa masikitiko.

Wakili huyo aliambia korti kwamba ni jambo la kustaajabisha kwamba wawekezaji sasa wanawindwa na polisi kupelekwa vizuizini badala ya kusaidiwa kuimarisha sekta ya uzalishaji mali.

Hakimu alielezwa mshtakiwa amefunguliwa mashtaka baada ya kushinda zabuni ya kununua kampuni ya saruji ya Bamburi Cement na ni jambo la kuvunja moyo na kuogofya.

Bw Miller alisema mshtakiwa hajafanya makosa yoyote na kwamba anadhulumiwa kwa sababu amefaulu kuininua Bamburi.

Mahakama iliombwa imwachilie mshtakiwa kwa dhamana aende hospitali kwa kuwa ana changamoto ya kiafya.

Hakimu aliahirisha uamuzi huo wa dhamana hadi Desemba 2, 2024.

“Sitaweza kutoa uamuzi sasa kwa vile naelekea katika Mahakama ya Kijeshi Eastleigh. Nitauandaa uamuzi huo na kuusoma Desemba 2, 2024,” Bw Shikwe alisema huku akiamuru mshtakiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga.

Baada ya mahakama kukabidhiwa agizo la mahakama kuu basi Bw Shikwe aliamuru mshtakiwa aachiliwe bila masharti.

Hakimu akasema: “Kufuatia agizo la mahakama kuu kuwa mshtakiwa aachiliwe bila masharti basi sina budi ila kutii. Mahakama hii iko chini ya mamlaka ya mahakama kuu.”

Bw Shikwe aliamuru kesi hiyo itajwe Januari 30, 2025 kwa maagizo zaidi.