Habari Mseto

Wataja ongezeko la mitumba kama kisiki cha ustawi wa sekta ya nguo

January 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

JAMES KARIUKI na CHARLES WASONGA

WATENGENEZAJI bidhaa nchini wamelalamikia ongezeko la nguo kuukuu maarufu kama mitumba zinazoingizwa humu nchini wakisema hali hiyo ni tishio kwa ustawi wa sekta ya utengenezaji bidhaa hizo.

Chama cha watengenezaji bidhaa (KAM) kimeitaka serikali kuongeza ushuru unaotozwa nguo hizo kama njia ya kuwezesha nguo zinazotengenezwa humu nchini kupata soko.

“Uagizaji mitumba kutoka nje ndio tisho kuu kwa watengenezaji wa nguo mpya humu nchini. Hii ndiyo maana tunaitaka serikali kuweka ushuru wa Sh2 milioni kwa kontena ya mitumba yenye urefu wa futi 20 na Sh4 milioni kwa kontena ya futi 40 ili kulinda mavazi yanayotengenezwa nchini kutokana na ushindani usio wa haki,” akasema afisa wa KAM.

“Na wale wafanyabiashara walaghai ambao huingiza nguo za mitumba nchini kupitia mipaka yetu wanafaa kutiwa mbaroni na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” akaongeza.

Nchini Kenya kuna jumla ya kampuni 170 za kutengeneza nguo, kuu miongoni mwazo zikiwa ni kampuni za Rivatex na Spinit zilizoko mjini Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu.