Kimataifa

Afrika yachagua rais wa pili mwanamke katika tukio la kihistoria

Na MASHIRIKA December 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WINDHOEK, NAMIBIA

RAIS mpya mteule wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah almaarufu NN amekuwa rais wa pili mwanamke kuchaguliwa Afrika.

Nandi-Ndaitwah anafuata aliyekuwa rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf aliyechaguliwa rais wa 24 na kutumikia Liberia kati ya 2006 na 2018.

Mbali na hayo, Nandi-Ndaitwah ndiye rais wa kwanza mwanamke kuchaguliwa nchini humo baada ya chama tawala cha SWAPO kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.

Akituma jumbe za pongezi, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alimpongeza Nandi-Ndaitwah kwa kuchaguliwa akisema ameweka historia ya kisiasa nchini humo.

Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa X, Rais Samia alisema, “Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, natoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais Mteule wa Jamhuri ya Namibia, kwa ushindi wako wa kihistoria katika uchaguzi mkuu wa Namibia wa 2024.”

Hii ni baada ya Tume ya Uchaguzi ya Namibia ECN, usiku wa kuamkia Jumatano kutangaza kuwa Nandi-Ndaitwah ambaye alikuwa makamu wa rais, ameshinda kwa zaidi ya asilimia 57 ya kura akifuatwa na mgombea wa chama kikuu cha upinzani Patriots for Change IPC, Panduleni Itula aliyepata asilimia 25.5 ya kura.

Japo Nandi-Ndaitwah ametangazwa mshindi wa uchaguzi huo, Itula na chama chake cha IPC walisema kwamba hawatambui matokeo ya uchaguzi huo ambao wanadai ulikumbwa na udanganyifu mwingi.

Aweka historia

Nandi mwenye umri wa miaka 72, sasa anakuwa mwanamke wa kwanza kuitawala nchi hiyo ya kusini mwa Afrika iliyo na utajiri wa madini.

Namibia imeongozwa na chama cha SWAPO tangu ilipopata uhuru mwaka 1990.

Zoezi la upigaji kura liliongezewa muda kutoka Novemba 27 hadi Novemba 30 baada ya matatizo ya kiufundi, ukiwemo uhaba wa karatasi ya kupigia kura kutokea, jambo lililoathiri mchakato wa kupiga kura.

Baadhi ya wapigakura walikata tamaa ya kupiga kura siku ya kwanza baada ya kusubiri kwa zaidi ya saa 12.

Chama cha IPC kilisema kwamba hii ilikuwa hatua ya kimakusudi na kwamba hakitakubali matokeo.

Shirika moja la mawakili wa haki za binadamu kusini mwa Afrika lililokuwa linahudumu kama mwangilizi wa uchaguzi huo pia lilisema hatua hiyo ya uhaba wa karatasi za kura na kucheleweshwa kwa zoezi la upigaji kura ilifanyika kimakusudi na kwamba lilitokea katika maeneo mengi.

Itula mwenye umri wa miaka 67 alisema wiki iliyopita kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na changamoto kadhaa.

Aliongeza kwamba chama cha IPC kitapambana kwa kutumia njia zote kuhakikisha kwamba zoezi zima la uchaguzi limefutiliwa mbali.

Tume ya Uchaguzi nchini Nambia ECN ilikiri kufeli katika maandalizi ya uchaguzi huo, ikiwemo upungufu wa karatasi za kupigia kura na hitilafu za mtandao.

ECN ilisema Jumanne kwamba kati ya watu milioni 1.5 waliojisajili kupiga kura, takriban asilimia 77 ndio walipiga kura.