The Gunners walivyozika Red Devils uwanjani Emirates
MASHABIKI wa Manchester United walipata jibu kuhusu nani mkali kati ya Arsenal na United baada ya vijana wa Mikel Arteta kuzika mashetani hao wekundu 2-0 kwenye Ligi Kuu (EPL) ugani Emirates kupitia mabao ya mabeki Jurrien Timber na William Saliba, Jumatano usiku.
Viongozi Liverpool nao walidondosha alama mbili katika sare ya 3-3 dhidi ya Newcastle ugani St James Park.
Bingwa mtetezi Manchester City walifufuka baada ya vichapo vinne mfululizo kwa kufyeka Nottingham Forest 3-0.
Nao Chelsea walirarua wenyeji Southampton 5-1, Wolves wakakunja mkia mikononi mwa Everton 4-0 ugani Goodison Park huku Brentford ikasalia bila ushindi ugenini katika mechi saba baada ya kupepetwa 3-1 na Aston Villa.
Arsenal walipata ushindi wao wa nne mfululizo dhidi ya United kwa mara yao ya kwanza katika historia baada ya Timber na Saliba kuona lango katika kipindi cha pili kutokana na mikwaju ya kona.
Mashetani wekundu wa United sasa hawana ushindi dhidi ya Arsenal mara saba mfululizo ligini katika uwanja wa Emirates.
Kichapo hicho ni cha kwanza cha kocha mpya wa United, Ruben Amorim.
Kona za kichawi
Red Devils walikuwa wamekoswa pembamba na Gabriel Martinelli na Thomas Partey, kabla Timber kufuma wavuni bao la kwanza dakika ya 54 kupitia kichwa baada ya kupokea kona kutoka kwa Declan Rice.
Amorim, aliyeonja ushindi wa kwanza EPL kwa kupiga Everton 4-0 mnamo Jumapili iliyopita, alifanya mabadiliko matatu kwa mpigo akiwaingiza Mason Mount, Joshua Zirkzee na Leny Yoro katika nafasi ya Marcus Rashford, Alejandro Garnacho na Harry Maguire, mtawalia.
Lakini Arsenal ndio walipata kuimarisha uongozi dakika ya 73.
Bukayo Saka alichota kona safi ambayo Partey alipiga mpira wa kichwa uliokamilishwa na Saliba.
Amorim alidai baada ya mechi kuwa Arsenal wanategea ikabu tu. Alisema mawinga Martinelli na Saka walitafuta kona kimakusudi.
Arteta alikiri kuwa ikabu ni baadhi ya silaha za Arsenal, lakini akapuuzilia mbali kuwa si silaha pekee.
“Sio tu ikabu. Wachezaji wengi wanaweza kujiundia mabao yao. Tunaweza kuunda nafasi ya kupata mabao kwa kupanga mechi, kuanzisha mchezo, kujibu mashambulizi na fursa za kupenya ngome ya wapinzani,” akasema Arteta.
Vijana wake walipata kona 13-0. Arsenal wamefunga magoli 22 kutokana na ikabu tangu msimu 2023-2024.
Reds watupa alama
Liverpool ya kocha Arne Slot ilipokonywa ushindi baada ya Fabian Schar kusawazisha 3-3 dakika za lala-salama.
Newcastle waliongoza mara mbili kupitia mabao ya Alexander Isak dakika ya 35 na Anthony Gordon (62) yaliyosawazishwa na Curtis Jones (50) na Mohamed Salah (68).
Salah kisha aliweka Reds juu 3-2 dakika ya 83 na kumpiku jagina Wayne Rooney katika kufunga na kutoa asisti ligini. Rooney alishikilia rekodi ya kuchangia bao na asisti katika mechi 36. Salah sasa amefanya hivyo katika michuano 37.
Schar alisawazisha dakika ya 90. Liverpool walidhani wamepata penalti dakika ya pili ya majeruhi Dan Burn alipozuia shuti la Alexis Mac Allister, lakini ikakataliwa na refa Andrew Madley pamoja na VAR.
Chelsea nao waling’oa Arsenal katika nafasi ya pili wakiongeza masaibu ya Southampton kupitia mabao ya Axel Disasi, Christopher Nkunku, Noni Madueke, Cole Palmer na Jadon Sancho.
Southampton walipata bao la kujifariji kutoka kwa Joe Aribo. Saints walicheza zaidi ya dakika 50 watu 10 baada ya Jack Stephens kulishwa kadi nyekundu.
Wolves nao walijifunga mabao mawili kutoka kwa Craig Dawson pamoja na kufungwa na Ashley Young na Orel Mangala mikononi mwa Everton.
Hatimaye Man City yaonja ushindi
Nambari nne City ya Pep Guardiola nayo ilinyoa Forest bila maji kupitia kwa mabao ya Bernardo Silva, Kevin De Bruyne na Jeremy Doku.
Villa walichana nyavu za Brentford kupitia mabao ya Ollie Watkins (penalti), Morgan Rogers na Matty Cash. Mikkel Damsgaard alifungia Bees goli la kufuta machozi.