Mashahidi wasimulia dhiki yao katika kesi ya mpango wa kusomea Finland
UKAKAMAVU wa Mary Chemutai ili kuwezesha mtoto wake kupata elimu bora ulimfanya ajitolee kwa kiwango ambacho kilimvunja moyo.
Lakini matumaini yake yalikatizwa na sasa anatafuta haki kortini.
Bi Chemutai ni mmoja wa mashahidi 202 katika kesi ambayo inamkabili Seneta Jackson Mandago na waliokuwa maafisa wawili wa kaunti, Mbw Joshua Leleo na Meshack Rono.
Wanashtakiwa kwa kula njama ya wizi na utumizi mbaya wa ofisi uliopisha ubadhirifu wa fedha.
Akishuhudia mbele ya Hakimu Mkuu Peter Ndege, Bi Chemutai alisimulia jinsi alikatiza elimu ya mwanawe katika Chuo Kikuu cha Presbyterian na kuuza mali yake ili kufadhili masomo chake ng’ambo.
Mpango wa ufadhili nje ya nchi ulivumishwa na serikali ya kaunti ya Uasin Gishu.
Mwana wake anayetambuliwa katika nyaraka za korti kuwa Benjamin, alikuwa mbioni kusoma katika nchi ya Finland.
Bi Chemutai alichukulia fursa hii kuwa nzuri kwa mtoto wake. Kulikuwa na ahadi ya kazi ng’ambo akiwa chuoni.
“Seneta Mandago, ambaye alikuwa gavana wakati huo, alituhimiza kuandaa pesa kwa muhula wa kwanza akiahidi kuwa watoto wetu wangelipa karo zilizosalia pindi watakapopata nafasi ya kusoma,” akasema.
Mahakama iliambiwa kuwa Bi Chemutai alilipa jumla ya Sh1.2 milioni kwa vipindi viwili; Sh550,000 Februari 2022, na malipo ya ziada ya Sh368,000.
Mnamo Septemba 6, 2022, alilipa Sh79,000 kupata pasipoti na bima ya afya na Sh80,000 ya nyumba.
Wakati huo, alikuwa amekabidhiwa barua ya mwaliko kujiunga na programu hiyo ya ufadhili lakini Benjamin hakuondoka nchini.
Kaunti hiyo ilizidi kuahirisha tarehe ya kusafiri mara kadhaa hadi Bi Chemutai akakata tamaa.
“Baada ya kuuza kila kitu, mtoto wangu hakusafiri na amekuwa nyumbani tangu nikatize masomo yake. Sina uwezo wa kumsajili katika chuo kingine kwa sababu sijabaki na chochote cha kuiba,” akasikitika.
Aliomba kurejeshewa hela zake kama alivyoshauriwa na maafisa wa mpango huo. Juhudi zake ziligonga mwamba.
Akihojiwa na mawakili wa washtakiwa, Bi Chemutai alipinga kuwa na ufahamu wa kozi ya awali kwa jina pathways studies ambayo ilikuwa ya lazima kabla ya kuenda Finland.
Wakili Stephen Kibungei alithibitishia korti kuwa sehemu ya pesa hizo zilikusudiwa kwa ada ya mitihani kabla ya kuidhinishwa na kusafiri.
Kulingana na Bw Kibungei, pesa zilizotolewa na Bi Chemutai zilikuwa za kufadhili elimu na kuandaa cheti cha usafiri na bima ya afya kabla ya mpango huo kukumbwa na changamoto.
Alidokeza kuwa kuna uwezekano mtoto wake alianguka mtihani wa utathmini kabla ya kusafiri.
Lakini Bi Chemutai alidai Benjamin alipita mitihani yote pamoja na mahojiano.
Zaidi ya mashahidi 35 walishuhudia katika kesi.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan