Makala

Wakazi wa Denyenye walia kuteswa na kubakwa kila mara na walinzi wa kampuni inayozozaniwa

Na Edwin Okoth, Ruth Hopkins December 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

KAMPUNI ya ulinzi inayofanya kazi katika kampuni ya kimataifa ya kutengeneza simiti na maafisa wa polisi walio katika ardhi kubwa inayozozaniwa, wamelaumiwa kwa kusababisha mateso, ubakaji na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu kwa wakazi kadhaa wa kijiji cha Denyenye, Kaunti ya Kwale.

Wanakijiji wanasema ardhi hiyo ya ekari 1,500 ni ardhi ya mababu zao lakini Bamburi Portland Cement Ltd inadai umiliki na inaanzisha kiwanda cha kusindika klinka katika eneo hilo.

Jamii ya Denyenye inadai walikumbana na ghasia kali kwa mara ya kwanza mnamo 1952, walipofurushwa kwa nguvu kutoka kwa ardhi ya mababu zao na serikali ya wakati huo ya kikoloni ya Uingereza.

Ardhi hiyo inadaiwa kuwa ilitolewa kwa afisa wa kijeshi aliyestaafu ambaye aliuzia Bamburi Cement mnamo 1954.Tangu wakati huo, kampuni hiyo ya kimataifa, ambayo inatumia ardhi hiyo kama eneo la hifadhi kwa shughuli zake za uchimbaji madini katika Kaunti ya Kwale, imewekeza kwa kutumia maafisa wa kupambana na fujo(GSU),pamoja na G4S, kampuni ya ulinzi ya kibinafsi kupiga doria katika ardhini kwa kutumia mbwa.Bw Shee Mbimbi ni mwenyeji wa eneo la Denyenye ambaye anafanya kazi kama mchimbaji madini.

Mnamo Agosti 2023, alikutana na walinzi wawili wa G4S alipokuwa akirudi nyumbani kutoka kwenye machimbo, akiokota vijiti vidogo njiani kutafuta kuni.Ndani ya dakika tano, Bw Mbimbi anadai, walinzi wawili wa G4S walimkabili na kumuuliza alikuwa akifanya nini.

Anadai mlinzi mmoja alianza kumpiga kwa fimbo, kabla ya mlinzi mwingine kumwachilia mbwa aliyemng’ata mguuni.’Kisha walinisindikiza nyumbani na kunionya nisimwambie mtu yeyote kwamba niliumwa na ‘mbwa wa Bamburi’,’ Bw Mbimbi alisema nje ya boma lake huko Denyenye.

Kaya bombo

Baadaye aliripoti shambulio hilo kwa polisi na kutembelea hospitali ya eneo hilo, lakini hakuweza kumudu matibabu, ikiwa ni pamoja na chanjo ya kichaa cha mbwa. Kanda ya video iliyonaswa moja kwa moja baada ya shambulio hilo inaonyesha Bw Mbimbi akihema kwa maumivu huku akieleza kilichotokea.

Anadai hakupelekwa katika kituo cha polisi lakini aliambiwa awaonye wengine wasiokote kuni kutoka shamba hilo iwapo hawataki mbwa waachiliwe kuwauma.Mwaka mmoja baadaye, jeraha la Bw Mbimbi limetoweka na linaonekana kutishia maisha.

Bado anakosa pesa za kulipia matibabu na anakabiliwa na uwezekano wa kukatwa mguu wa kushoto.Gazeti la Taifa Jumapili limeona ripoti sita za polisi na kuzungumza na wanakijiji kadhaa ambao wanadai kuwa wameshambuliwa na walinzi hao, wengine kwa kuumwa na mbwa mara kadhaa.

Wanakijiji wako hoi hata zaidi kabla ya maafisa wa polisi wa GSU waliokuwa na silaha kufika Denyeye mwaka wa 1997, wakati mapigano ya ‘Kaya Bombo’ yalipokuwa yamechacha. Maafisa hao wako walitumwa katika shamba hilo na maafisa 30 wanaendelea kuwepo muda mrefu baada ya mapigano kumalizika.

Wanakijiji wanasema uwepo wao umeongeza maumivu zaidi badala ya ulinzi.Bi Mwakideu (si jina lake halisi), anadai amebakwa mara mbili katika miaka minne na maafisa wa GSU. Anadai alipata mtoto wa kike kutoka kwa ubakaji wa kwanza mnamo 2011.

“Wakati GSU ilipotukabili, nilibakwa na ni siri niliyoapa kupeleka kaburini kwangu. Nilipata mimba na kumzaa msichana ambaye sasa ana umri wa miaka 13. Mume wangu aliniacha baada ya kujua kilichonipata. Yeye (binti) hayuko shuleni sasa kwa sababu sina pesa za kumsomesha,” anasema.

Miaka minne baadaye, anadai alikumbana na hali kama hiyo aliporudi kutafuta kuni za kupikia.

Wanawake wengi

“Nilihisi vibaya sana kwa sababu tumekuwa tukichota kuni katika msitu huu tangu utoto wangu. Sikuripoti kwa polisi kwa sababu tulikuwa tumeambiwa kwamba huwezi kamwe kuripoti GSU au kuwapeleka mahakamani,” asema, akiongeza kuwa wanawake wengine wengi wamepitia tukio kama hilo lakini wanaona aibu sana kusema.

Akisukumwa na umaskini, Bi Mwakideu bado anaenda kutafuta kuni msituni. Amewazia kuandamana na bintiye mwenye umri wa miaka 13 lakini uwezekano wa mtoto huyo kudhuriwa umemzuia.Mishi Juma anadai kuwa mwanawe alifariki baada ya kupigwa na maafisa hao waliomkamata mwaka 2004 alipokuwa akichota kuni.

“Niliambiwa kuwa maafisa wa GSU walimshukia na kumpiga. Ndugu zake walimbeba hadi nyumbani. Tulimpeleka katika hospitali ya Kwale, ambapo siku ya tatu alifariki. Madaktari walipata mbavu zake zilikuwa zimevunjwa kutokana na mateke ya maafisa hao. Sikuweza kufanya mengi (kulalamika), hasa baada ya baba yake kufariki. Tumeambiwa kila mara kuwa huwezi kumshtaki afisa wa polisi na kushinda kesi mahakamani,” Bi Mishi, 60, alisema.

Hivi majuzi zaidi, Kwale Mining Alliance (KMA), shirika la kiraia linalotetea haki za wakazi wa Kwale wanaoishi karibu na maeneo ya uchimbaji madini walijaribu kumwokoa Bw Juma Sudi Mwamkungoma baada ya kudaiwa kupigwa na GSU.

Alikuwa ameingia katika shamba la Bamburi mnamo Agosti 30, 2023 kutafuta kuni, lakini maafisa watatu wanadaiwa kumkamata na kuamuru kupeleka kuni hizo katika kambi ya GSU. Huko, aliiambia KMA kwamba maafisa watatu na mkuu wao walimpiga.Shirika hilo liliandamana na Bw Mwamkungoma hadi kituo cha polisi, ambapo aliripoti shambulio hilo.

Mahojiano ya video

Taifa Leo imeona nakala ya ripoti hiyo na mahojiano ya video ambapo KMA ilizungumza naye mnamo Septemba 9, 2023. Alikufa mnamo Septemba 20.Tuliwaandikia polisi wa Kenya na Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi kuhusu madai haya lakini hakuna aliyejibu licha ya kufuatilia mara nyingi.

G4S, kampuni ya kimataifa ya usalama ya kibinafsi ya Uingereza iliyonunuliwa mwaka wa 2021 na kampuni ya usalama ya Amerika ya Allied Universal, ilikanusha makosa yoyote ya maafisa wake. Badala yake walishutumu baadhi ya waathiriwa wanaodaiwa ‘kuvamia mbwa wao’ waliokuwa wakishika doria.

Bamburi Cement, ambayo ni sehemu ya LafargeHolcim (moja ya makampuni makubwa ya kimataifa ya vifaa vya ujenzi duniani), ilisema haijathibitisha madai yoyote yaliyotolewa na wanakijiji.

“Kampuni haijapata ushahidi wa makosa baada ya kufanya uchunguzi na maswali. Bamburi imejitolea sana kuheshimu viwango vya kimataifa kuhusu haki za binadamu, kama vile Mwongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Kibinadamu,” kampuni hiyo iliandika kujibu orodha ndefu ya maswali.

Jamii ya eneo hilo inadai kwamba Bamburi haikuwashirikisha katika mpango mpya wa kutumia ardhi ya mababu zao inayozozaniwa, ambayo wanaiita ‘Chikuyumtole’. hatua wanayodai haikuwa halali kwa vile ardhi iliyo karibu na ufuo huo inachukuliwa kuwa ya umma.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA