Habari za Kitaifa

Usafiri kutatizika msimu wa sikukuu barabara 2 kuu zikifungwa Nairobi

Na BENSON MATHEKA December 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAMLAKA ya Kitaifa ya Barabara Kuu (KeNHA), imetangaza kuwa madereva wanaotumia barabara kuu ya Nairobi-Nakuru wanapaswa kutarajia kutatizika kuanzia katikati ya Desemba hadi Januari 2025.

Kulingana na mamlaka hiyo, usumbufu huo umetokana na ujenzi katika sehemu ya Barabara ya Waiyaki katika makutano ya Kangemi, ambayo itafungwa kwa muda kuanzia Desemba 11 hadi Januari 17, 2025 kwa ujenzi wa daraja la kuunganisha barabara za Loresho, Muthanga na Hinga.

“Tungependa kufahamisha umma kuhusu kukatizwa kwa trafiki kwa muda katika makutano ya Kangemi kwenye Barabara Kuu ya A8 (Waiyaki),” mamlaka hiyo ilisema.

Kufungwa kwa barabara hiyo kwa siku 37 kutatekelezwa kwa awamu mbili, ya kwanza itaathiri madereva wa magari wanaoelekea Nairobi. Awamu ya 1 itatekelezwa kuanzia Jumatano, Desemba 11, 2024 hadi Jumatatu, Desemba 26, 2024.

Awamu ya 2 itatekelezwa kuanzia Jumamosi Desemba 28, 2024 hadi Ijumaa Januari 17, 2025.Mamlaka hiyo iliwashauri madereva kufuata mpango uliopendekezwa wa usimamizi wa trafiki na kushirikiana na polisi na wakuu wa trafiki.

Katika tangazo tofauti, KeNHA ilisema barabara kuu ya Thika Superhighway pia itafungwa kwa kiasi kuanzia Desemba 12 hadi 17.Mamlaka hiyo ilisema barabara hiyo itafungwa katika eneo la Juja Highpoint (Centurion) ili kuruhusu ujenzi wa daraja la wanaotembea kwa miguu.