Gachagua abuni mikakati mipya ya kujihakikishia usalama na kuwafikia wafuasi
NAIBU Rais aliyeondolewa mamlakani Rigathi Gachagua ameamua kuepuka kuonekana hadharani na kuanza kutumia mbinu ya kupiga simu wakati wa hafla za umma eneo la Mlima Kenya kufuatia shambulizi ya hivi majuzi akiwa mazishini huko Limuru.
Bw Gachagua amekuwa akipiga simu zinazowekwa kwenye vipaza sauti, kuzungumza katika hafla huku akizingatia usalama wake kufuatia shambulio hilo ambalo washirika wake wametaja kama jaribio la mauaji.
Katika mashambulio yake ya kisiasa dhidi ya Rais William Ruto baada ya tofauti zao zilizosababisha kuondolewa madarakani, Bw Gachagua anaonekana kutumia mpango madhubuti unaohusisha kujitokeza bila kutangazwa kibinafsi hadi kuonekana kwenye sherehe za muziki na kusaidia walio katika dhiki kupitia michango ya pesa.
Wadadisi wanasema kuwa lengo kuu la Bw Gachagua ni kusalia katika mawazo ya umma huku akiimarisha uungwaji mkono eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapigakura kabla ya uchaguzi wa 2027.
Mahali popote kunakofanyika hafla inayohudhuriwa na watu wengi katika Mlima Kenya, kuna mtindo unaoibuka wa mshirika wa Gachagua kuandaa jukwaa kwa naibu wa rais wa zamani kuhutubu.
Kwa kawaida washirika wake huwa wanapiga simu na kuiunganisha na vipaza sauti ili Bw Gachagua ahutubie umati. Mnamo Novemba 28, 2024 Bw Gachagua alitembelea kimyakimya nyumbani kwa mwanamuziki mkongwe wa benga Daniel Kamau maarufu kwa jina la kisanii (DK) wa Maria katika eneobunge la Gatanga.
Hawataweza
Alitangaza kwamba ‘kuna njia nyingi za kuchuna paka ngozi na ikiwa watu wataendelea kujitolea kwa ukombozi wetu kutoka kwa utawala mbaya tutakuwa washindi’.
Bw Gachagua alitarajiwa baadaye Desemba 4, 2024 kufika katika hafla ya mazishi Kaunti ya Kirinyaga kupitia simu.MCA wa Baragwi David Mathenge alipoalikwa kuhutubia waombolezaji, alitangaza kwamba alikuwa akichangia wakati wake kwa Bw Gachagua.
“Ninataka kuwatangazia kuwa Bw Gachagua yuko hapa pamoja nasi na atawahutubia baada ya muda mfupi. Nenda uwaambie wale wanaofikiri wanaweza kufika popote na kuzua vurugu hawataweza,” Bw Mathenge alisema.
Alimpigia simu Bw Gachagua na kumweka kwenye vipaza sauti akazungumza na umma. Bw Gachagua aliwashukuru waombolezaji waliokuwa wakishangilia na kuwaambia kwamba bado amejitolea kuokoa nchi kutokana na kile alichokitaja kuwa utawala wa ‘kujipiga vifua.’
Bw Gachagua alisema pia anafurahi kwamba wakazi wa Mlima Kenya wanaongoza vita dhidi ya utawala mbaya na kutekwa kwa serikali.Bw Rigathi amekuwa akijitokeza katika misafara inayoandaliwa na washawishi wa mitandao ya kijamii na ambayo huvutia umati mkubwa.
Katika hali kama hizi, mratibu humwita naibu rais atoe hotuba kupitia simu.Shambulio la Limuru lilijiri baada ya Katibu wa kibinafsi wa Bw Gachagua Mumbi wa Munene mnamo Oktoba 25, 2024 kuliambia Taifa Jumapili kwamba serikali ilikuwa imeondoa kikamilifu usalama wa naibi rais huyo wa zamani.
Sasa, Bw Gachagua na wafuasi wake wanaonekana kutumia mikakati inayolenga kupata fursa ya kutangamana na wafuasi wake hata ikidhihirika kuwa serikali inajitahidi kumzuia.
Kulingana na Mbunge wa Githunguri Bi Gathoni wa Muchomba, wale wote wanaompenda Gachagua wataandamana hadharani ikihitajika kusitisha mateso dhidi ya mbunge huyo wa zamani wa Mathira. Bi Muchomba aliambia Taifa Leo kuwa ‘tunataka washirika wetu wote wa maendeleo na demokrasia kuzingatia kwamba kuna kiongozi nchini Kenya anayeteswa kwa kupinga ufisadi, udikteta, utekaji nyara na mauaji ya kiholela.’
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA