Habari za Kitaifa

Kindiki asema serikali imefungwa mikono kuhusu kuunda IEBC

Na SHABAN MAKOKHA, VICTOR RABALLA December 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki Jumapili alisema kuwa vikwazo vya kisheria ambavyo vinachelewesha kubuniwa kwa jopo la kuwateua Makamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) vinastahili kuondolewa.

Profesa Kindiki alisema demokrasia ya Kenya iko pabaya iwapo IEBC haiwezi kutekeleza wajibu wake. Alisema hatua ya kuwasilishwa kwa kesi ya kupinga kubuniwa kwa jopo la uteuzi wa makamishina wa IEBC kunatatiza mchakato wa maandalizi ya uchaguzi wa 2027.

Pia aliongeza kuwa kuna wadi na maeneobunge ambako wawakilishi wao waliaga dunia lakini chaguzi ndogo hazijaandaliwa kutokana na IEBC kutokuwa na idadi tosha ya makamishina na mwenyekiti.

“Kama serikali mikono yetu imefungwa kutokana na amri ya korti. Kutokana na hilo tunawaomba Wakenya ambao walielekea kortini waondoe kesi hiyo ili mchakato wa kuteuliwa kwa makamishina wapya wa IEBC uendelee,” akasema Profesa Kindiki.

Alikuwa akiongea katika Shule ya Upili ya Chebuyusi eneobunge la Navakholo wakati wa ibada ya Jumapili. Alisisitiza kuwa serikali inataka sana IEBC iwe na idadi tosha ya makamishina na mwenyekiti ili irejelee shughuli zake lakini wamefungwa mikono.

Raia Boniface Njogu alielekea kortini mnamo Oktoba mwaka huu kupinga uteuzi wa jopo la kuwapiga msasa na kuwateua makamishina wa IEBC.

Alisema walemavu hawakuwakilishwa kwenye jopo ambalo lilinuiwa kubuniwa.

Kesi hiyo itaamuliwa mnamo Januari 2025.

Awali kulikuwa na utata kuhusu mwakilishi wa Azimio kwenye jopo hilo kati ya Wiper na chama cha NLP kuhusu nani alistahili kutoa mwakilishi kwenye jopo hilo.

Hata hivyo, hilo lilitatuliwa na NLP kupewa nafasi hiyo. Mchakato wa kuwapata makamishina wapya wa IEBC unatarajiwa kuanza baada ya jopo kubuniwa.