Habari Mseto

Mshauri wa Rais ataka wanawake waungane kusuluhisha changamoto zao

Na GEOFFREY ANENE December 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MSHAURI wa Rais kuhusu masuala ya watoto na wanawake Harriet Chiggai ameyarai makundi mbalimbali ya wanawake yashiriki miradi inayowainua ili kukabili changamoto zinazowaandama kwenye jamii.

Bi Chiggai amesema kuwa siku 16 ambazo ni za uanaharakati kuhusu haki na kutomeza dhuluma za kijinsia, zinastahili zitumike kuwazia jinsi ambavyo wanawake watajiinua na kufanikiwa maishani.

Kumekuwa na vifo 97 vinavyotokana na dhulima za kijinsia na Bi Chiggai anasema kuwa wale ambao wamelengwa sani ni wanawake na wasichana matineja.

“Haya mauaji yanastahili yakome kwa sababu hayasawiri kabisa utu na heshima kwa uhai wa binadamu. Hali hii inazua wasiwasi kuhusu usalama wa wasichana na watoto wetu nyumbani,” akasema Bi Chiggai.

Alikuwa akiongea Jumapili katika uwanja wa Kirigiti Kaunti ya Kiambu ambapo wanawake walishiriki mashindano ya ulengaji shabaha.

“Kila mtu lazima ashiriki juhudi za kupata suluhu kwa suala hili. Kanisa lina jukumu, spoti ina wajibu na kama jamii lazima tufanye wajibu wetu kuhakikisha wanawake hawahofii usalama wao na kuuawa kinyama,” akaongeza.

Alishukuru kila mtu ambaye amejitokeza kuzungumzia mauaji ya wanawake ambayo yamekuwa yakiripotiwa huku akisema ni wanawake tu ndiyo watasababisha baadhi ya wanaume katili wabadilike.

Aidha aliongeza kuwa baadhi ya mauaji hayo yanatokana na tamaduni na fikira potovu za kiakili kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii. Wakati huu ambapo shule zimefungwa, Bi Chiggai alishauri wazazi wamakinikie malezi ya watoto wao ambayo kwa sehemu kubwa hufanywa na walimu wakiwa shuleni.

Mashindano hayo ya ulengaji shabaha yaliyowaleta pamoja wanawake kutoka idara mbalimbali za serikali na sekta ya kibinafsi yaliandaliwa na Paula Munyi ambaye ni mwanzilishi wa kundi la wanawake wanaoshiriki ulengaji shabaha maarufu kama Pink Target Ladies Sports Shooting Club.

“Mwaka jana tuliandaa hamasisho kuhusu kansa ya matiti na mwaka huu ni kuhusu dhuluma ya kijinsia. Huwa tunatumia mchezo huu kuja pamoja kama wanawake kusaidia kupambana na changamoto mbalimbali za kijamii,” akasema Bi Munyi.