Akili Mali

Sababu za bei ya mafuta ya kupikia kupanda huku ya petrol ikishuka 2024

Na BENSON MATHEKA December 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BIDHAA muhimu zikiwemo za nyumbani mapema mwaka huu, zilikuwa zikiuzwa kwa bei ya juu huku bei za baadhi ya bidhaa zikishuka kwa kiasi mwaka ulivyosonga.

Hata hivyo, baadhi ya bidhaa ambazo zilitarajiwa kushuka kwa bei ya rejareja kama vile mafuta ya kupikia zilikaidi matarajio na kupanda juu kidogo.

Mabadiliko haya ya bei yaliathiri bei ya mafuta ya petroli pia, na kuwaacha Wakenya wakiwa wamechanganyikiwa kuhusu mabadiliko hayo.

Benki Kuu ya Kenya (CBK) mnamo Jumatatu, Desemba 9, ilitoa ufafanuzi kuhusu ripoti yake ya Sera ya Fedha ya mwisho wa mwaka ikielezea mabadiliko ya bei na nini cha kutarajia.

Bei ya mafuta ya kupikia iliongezeka mnamo Oktoba 2024 na kuna uwezekano itaendelea kupanda hadi mwaka ujao kutokana na sababu zinazoanzia bara Asia.

Lita 10 za mafuta ya kupikia sasa ni takriban Sh2,650 kutoka Sh2,000 huku lita tatu zikiuzwa Sh900.

CBK ilifichua kuwa bei ya mawese, soya na alizeti ilichangia kupanda kwa sababu ya kupungua kwa uzalishaji katika nchi muhimu Kusini-mashariki mwa Asia.

”Mfumko wa bei ya mafuta ya kupikia uliongezeka mnamo Oktoba 2024, ukichangiwa na bei ya juu ya mawese, soya na alizeti, kutokana na kupungua kwa uzalishaji katika nchi zinazozalisha mafuta Kusini-mashariki mwa Asia,” ilisema ripoti ya CBK.

Kenya kwa mara ya kwanza ilipiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje mwaka huu baada ya uzalishaji wa ndani kuongezeka hadi kiwango kinachoweza kukidhi nchi kwa mwaka.

Kulingana na ripoti ya Sera ya Fedha ya CBK, bei ya petroli ilipungua mwaka huu licha ya mzozo mkubwa wa kisiasa katika Mashariki ya Kati ambako kuna mataifa mengi yanayozalisha mafuta kwa wingi.

Bei hizo pia zilisalia kuwa tulivu huku lita moja ya petroli, dizeli na mafuta taa ikiuzwa Ksh180.66, Ksh168.06. na Ksh151.39 mtawalia, na kuna uwezekano wa kusalia hivyo kutokana na kuongezeka kwa usambazaji kutoka kwa nchi sio wanachama wa Shirika la Nchi Zinazozalisha Mafuta ya Petroli (OPEC) na mahitaji ya chini China.