Makala

Jamhuri 2024: Kindiki amsifia Ruto kwa kusaka Raila na Kenyatta

Na SAMMY WAWERU December 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU Rais Kithure Kindiki amemmiminia sifa bosi wake, Rais William Ruto akimtaja kama kiongozi “anayethamini umoja wa nchi” kwa kuunda serikali jumuishi. 

Prof Kindiki, akihutubu Alhamisi, Desemba 12 wakati wa maadhimisho ya Jamhuri Dei 2024, alisema hatua ya Rais Ruto kuunda serikali jumuishi – inayoshirikisha upinzani, imeleta utangamano wa taifa.

“Kwa kufikia washirika wote (akimaanisha mrengo wa upinzani ulioongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga), ni ishara unathamini umoja wa taifa,” Prof Kindiki alisema.

Maadhimisho ya Jamhuri 2024 yalifanyika Uhuru Gardens, Nairobi, na naibu rais alitumia jukwaa hilo kusifia Dkt Ruto kwa kushirikisha Bw Raila kwenye serikali ya Kenya kwa kuteua baadhi ya wandani wa Waziri Mkuu huyo wa zamani kujiunga na Baraza la Mawaziri.

Prof Kindiki alitaja hilo kama hatua muhimu kwa nchi kujumuisha washirika wote kwenye utendakazi wa serikali.

Majuzi, Ruto alitembelea Rais mstaafu Uhuru Kenyatta nyumbani kwake Ichaweri, Gatundu, Kiambu ambapo wawili hao walijadili kuhusu masuala ya nchi.

“Tunakushukuru kwa kumfikia Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, na kuenda mbele kila mmoja anapaswa kuhusishwa kwenye masuala ya uboreshaji taifa,” Kindiki alisema.

Prof Kindiki aliteuliwa miezi michache iliyopita kuwa naibu wa rais, baada ya mtangulizi wake, Rigathi Gachagua kubanduliwa.

Bw Gachagua alikuwa mgombea mwenza wa Ruto katika uchaguzi mkuu 2022, ambapo walitumia tikiti ya Kenya Kwanza kumenyana na Raila Odinga (Azimio la Umoja).