Dimba

Pesa ‘iligulwa’: Vimbwanga vya uchaguzi wa FKF vyachipuka

Na CECIL ODONGO December 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAKOVU ya kupoteza uchaguzi yanaendelea kuchipuka wiki moja baada ya kura za Shirikisho la Soka Nchini (FKF), Mwenyekiti wa Kakamaga Homeboyz Cleophas Shimanyula akiwa wa hivi punde kutoa makeke yake.

Shimanyula ambaye alipata kura nne na kubwagwa na Rais mpya Hussein Mohamed, Alhamisi aliitisha Sh50,000 ambazo alikuwa ameipa Luanda Villa ikidaiwa klabu hiyo haikumpigia kura kwenye uchaguzi huo.

Inadaiwa Shimanyula alikuwa amehakikishiwa kura za mwenyekiti Moses Abwenje lakini akaishia kuunga mkono mrengo wa Mohamed.

“Pesa hizo awali zilikuwa zimetumwa na Shimanyula kusaidia klabu kugharimia mechi yake ya kule Mombasa. Hata hivyo, kutokana na matokeo ya uchaguzi mkuu, Shimanyula aliomba tumrejeshee pesa zake na tumefanya hivyo,” ikasema taarifa iliyotiwa saini Ambwenje.

Afisa huyo aliambatisha ithibati kuonyesha wamerejeshea Shimanyula hela zake na wakamshukuru kwa nia yake ya awali ya kusaidia klabu.

Kutokana na hatua ya Luanda Villa, madai yamezuka kuwa waliokula pesa za Shimanyula wakati wa kampeni na hawakumpigia kura wameanza kuingiwa na tumbo joto.

Si Luanda Villa pekee bali ndani ya Gor Mahia, Katibu Mkuu Sam Ochola amejipata pabaya mashabiki wa klabu wakimlaumu kwa kumkaidi mlezi wa klabu na kigogo wa siasa nchini Raila Odinga, na kuunga Doris Petra dakika za mwisho.

Mashabiki wa Gor walimkemea Ochola wakimtaka ajiuzulu na wengine wakimuonya kuhudhuria mchuano wowote wa klabu.

Akizungumza na Taifa Spoti, Ochola alikana vikali kumuunga Petra na akasema alikuwa debeni hata kama hakupigiwa kura.

Kuonyesha kulikuwa na mgawanyiko kambi ya Gor kuelekea kura hiyo wikendi jana, hata Gerphas Okuku aliyekuwa na kura ya K’Ogalo hakumpigia katibu huyo.

“Sisi kama wawaniaji wenye asili ya Kiluo tulikutana na Raila akaturuhusu tuelewane mtu wa kuunga kati yetu. Hata hivyo, hatukuwa tumeelewana na wakati tulirejea kwake (mkesha wa uchaguzi), alikuwa ameelekea Djibouti,” alihoji Ochola.

“Kama sikupigiwa kura basi mwenye alikuwa na kura ya Gor ndiye anafaa kujibu hilo. Hata hivyo, hakuna mahali niliunga mkono Petra. Nilikuwa debeni ila nikakosa kuchaguliwa,” akaongeza Ochola.

Haya yanatokea wakati imefichuka baadhi ya wajumbe walioshiriki uchaguzi huo uwanjani Kasarani, Nairobi, walichukua hongo kutoka wawaniaji mbalimbali lakini ilipofika kura waliwageuka.

Katibu huyo alisisitiza suala la uchaguzi halifai kutumika kumpiga vita Gor huku akirai umoja miongoni mwa wadau ili watathmini utendakazi wa ofisi mpya ya FKF.

“Soka Kenya ina matarajio mengi. Kwetu sasa ni kuweka macho na kuhakikisha Mohamed na wenzake wanainua soka kama walivyoahidi,” alihoji.

Haya yanatokea wakati imefichuka baadhi ya wajumbe walioshiriki uchaguzi huo uwanjani Kasarani, Nairobi, walichukua hongo kutoka wawaniaji mbalimbali lakini ilipofika kura waliwageuka.