Matumizi ya wadudu na shayiri kupunguza gharama ya ufugaji kuku
KWA zaidi ya miongo miwili ambayo Joyful Birds Self-Helf Group imekuwa ikifugaja kuku, imeshuhudia changamoto za hapa na pale kuendeleza biashara hiyo.
Kando na kuondolewa sehemu ambayo walikuwa wamewekeza pakubwa mwezi Aprili mwaka huu, 2024, kufuatia ubomoaji wa majengo yaliyo karibu na mito Nairobi, mfumko wa bei ya chakula cha mifugo nusra uzime bidii za kundi hilo la wanachama 21.
Linaendeleza ufugaji wa kuku wa kienyeji walioboreshwa na wale halisi, katika mtaa wa mabanda wa Soweto, Kayole, Nairobi.
Awali, lilikuwa limejenga vizimba karibu na Mto Soweto, japo amri ya serikali majengo na makazi yaliyo karibu na mito ya jiji yabomolewe iliwaathiri.
Timothy Malasi, mwenyekiti, anasema gharama ya chakula cha kuku ingali kikwazo kwa wafugaji wengi, ila Joyful Birds ina siri.
“Mbali na kutegemea malisho ya madukani, tumekumbatia matumizi ya shayiri na wadudu maalum aina ya BSF,” Malasi anadokeza.
Ni chakula mbadala kinachochukua siku chache kuandaa.
Kulingana na Zadock Ambuka, karani na msimamizi wa malisho, shayiri (barley) huchukua muda wa siku saba pekee kukomaa.
“Wadudu aina ya BSF (ndio Black Soldier Fly), huchukua siku 14 tu,” Ambuka akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano katika mradi huo Soweto, Kayole.
Mbinu hizo zinazowapa wafugaji afueni, Joyful Birds Self-Helf Group inakiri zimeipunguzia gharama kwa karibu asilimia 50.
Kwa sasa lina zaidi ya kuku 600.
Hali kadhalika, kundi hilo linafuga kanga, bata mzinga na kware.
Limejikita sana kwa kufuga kuku wa nyama na mayai, Malasi akihoji uzalishaji wake hautoshi mahitaji ya soko Kayole.
Covid ilipotua Kenya 2020, janga hilo la kimataifa lilichochea gharama ya chakula cha mifugo kupanda bei mara dufu.
Malisho ya kuku ya madukani ndiyo yameathirika zaidi.
Wafugaji wanahimizwa kukumbatia mbinu mbadala kuunda chakula, ili kushusha gharama.