Habari

Afueni msimu wa Krismasi bei ya mafuta ikipungua

Na CHARLES WASONGA December 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imewapa afueni wenye magari na Wakenya kwa jumla msimu huu wa sherehe kwa kupunguza bei ya petroli, dizeli na mafuta taa.

Kwenye taarifa Jumamosi, Mamlaka ya Kudhibiti Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) ilieleza kuwa bei ya petroli imepungua kwa Sh4.37 kila lita huku dizeli na mafuta taa zikishuka Sh3 kwa lita moja, mtwalia.

Hii ina maana kuwa jijini Nairobi na viunga vyake, petroli itauzwa bei ya rejareja ya Sh176.29 lita moja kutoka Sh180.66 kati ya Novemba 15-Desemba 14, 2024.

Nayo dizeli itauzwa Sh165.06 kwa lita kutoka Sh168.06, mafuta taa yakiuzwa Sh145. 15 kila lita kutoka Sh151.39 mwezi jana mtawalia.

Mhudumu akitia mafuta kwa gari katika kituo kimoja mjini Nyeri mapema Januari 2024. Bei za dizeli, petroli na mafuta taa zimepungua kwa Sh3 wastani kuelekea sikukuu ya Krismasi. PICHA | JOSEPH KANYI

Mjini Nakuru petroli itauzwa Sh175.51, dizeli Sh164.63 nayo mafuta taa Sh148.01 kwa lita.

Katika miji ya Eldoret na Kisumu, wenye magari watanunua petroli Sh176.33 kwa lita, dizeli Sh165.45 nao watumiaji mafuta taa watayapata kwa Sh148.82 kila lita.

“Bei hizi mpya zitaanza kutumika kuanzia Desemba 15, 2024 hadi usiku wa manane Januari 14, 2025,” Epra ilieleza kwenye taarifa yake.

Mamlaka hiyo iliongeza kuwa bei hizo mpya zinajumuisha ushuru wa thamani ya bidhaa (VAT) wa asilimia 16 kuambatana na hitaji la Sheria ya Fedha 2023 na sheria zingine husika.

Epra iliongeza kwamba bei ya petroli ilipungua kwa kima cha asilimia 4.46 kutoka dola 641.14 (Sh83.348.2) mwezi Oktoba hadi dola 612.53 (79,628.9) kwa lita 1000 mwezi Novemba 2024.