Mutuse afichua zawadi aliyopewa baada ya kumtimua Gachagua
MBUNGE wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, kwa mara ya kwanza amefichua kuwa ni Rais William Ruto aliyempa kibarua cha kuwasilisha hoja ya kumtimua aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Na mshahara wa kazi hiyo, akaeleza, ni mpango mpya wa serikali wa kuweka lami barabara ya Emali-Ukia, inayopita katikati mwa kaunti ya Makueni.
Itakuwa mradi wa kwanza kutekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza kaunti hiyo tangu Rais Ruto alipoingia mamlakani Septemba 22, 2022.
Bw Mutuse, akasema: “Kuwekwa lami barabara hii muhimu ni tunu kutoka kwa Rais William Ruto kwangu baada ya kuwasilisha na kuwezesha kupitishwa kwa hoja ya kumtimua Rigathi Gachagua.”
“Bw Gachagua alikuwa anapanga kupeleka Sh2 bilioni ambazo serikali ilipata kutoka China, hadi eneo la Mlima Kenya kufadhili uwekaji lami barabara ya Mau Mau. Nilipofaulu kumwondoa mamlakani, sasa Rais ameniambia serikali itaweka lami barabara ya Emali-Ukia,” Bw Mutuse akawaambia waombolezaji katika kijiji cha Muatini.
Alisema hayo wakati wa mazishi ya Mama Naomi Mulatya, mamake Florence Mulatya, aliyekuwa mwakilishi wa kitengo cha Elimu katika ubalozi wa Kenya Australia.
Ilikuwa ni mara kwanza kwa Bw Mutuse aliyechaguliwa kwa chama cha Maendeleo Chap Chapa, kuzungumzia mchakato wa kuondolewa mamlakani kwa Bw Gachagua, shughuli iliyomweka kwenye ramani ya kitaifa.
Mbunge huyo alimsuta Bw Gachagua kwa kuendeleza ukabila na kuhujumu maendeleo katika eneo la Ukambani. Tangazo la Mutuse liliwachangamsha wakazi japo wengine walikuwa na shauku.
“Hii itakuwa mafanikio makubwa ya serikali hii katika kaunti ya Makueni. Tumesubiri kwa miongo mingi,” akasema George Mutinda.
“Kila Desemba sisi huambiwa kuwa barabara hi itawekwa lami Februari mwaka unaofuata. Tumezoea ahadi kama hizi,” akasema Charity Wavinya Mwalimu.
Wakati ambapo hoja ya kumtimua Bw Gachagua ilikuwa ikijadiliwa na mashtaka 11 kujadiliwa, wabunge walioipinga walidai Bw Mutuse hakuelewa yaliyomo.
“Huyu Mutuse sio mmiliki wa hoja hii kwa sababu haelewi chochote kuihusu. Mmiliki kamili wa hoja hii sio mwingine ile Rais William Ruto,” akasema Mbunge wa Mukrwe-ini John Kaguchia mnamo Oktoba 8, 2024 kabla ya hoja hiyo kupigiwa kura katika Bunge la Kitaifa.
Na katika Bunge la Seneti, Bw Mutuse alikabiliwa na wakati mgumu alipodadisiwa na mawakili wa Bw Gachagua wakiongozwa na Ndegwa Njiru.
Mara kadha, Mbunge huyo wa Kibwezi Magharibi alionekana kulemewa na makombora ya maswali kutoka kwa mawakili hao.
Barabara hiyo ya Emali-Ukia, ni sehemu ya barabara kuu inayounganisha Tanzania na Ethiopia, kupitia kaunti kadhaa, ni yenye umuhimu mkubwa kwa wakulima wa matunda katika kaunti ya Makueni.
“Kuwekwa lami kwa barabara ya Emali-Ukia kutaweka pesa mifukoni mwa wakulima wa matunda kwa sababu wataweza kufikisha mazao yao sokoni mwa urahisi,” Spika wa Bunge la Kaunti ya Makueni Douglas Mbilu akasema juzi.
Wakati wa kampeni ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, mradi wa uwekaji lami barabara hiyo ni miongoni mwa ile ambayo Rais Ruto na kiongozi wa Azimio Raila Odinga waliahidi kutekeleza kwa manufaa ya wakazi wa Makueni.