Dondoo

Pasta achomea boda picha kwa demu wake na kuvuruga harusi

Na CORNELIUS MUTISYA December 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

PASTA alivuruga harusi ya jamaa muongo alipomwanika kwa mchumba wake na marafiki.

Kulingana na mdaku wetu, polo alikuwa amehadaa kidosho kwamba ameajiriwa katika shirika moja la fedha mjini kumbe ni mwendeshaji bodaboda mjini Uani, Machakos.

“Polo alikutana na demu katika pilkapilka zake mtaani. Akamhadaa kwamba anafanya kazi nzuri yenye pesa nono. Uhusiano wa kimahaba ukaota na wakaamua kufunga ndoa,” alieleza mdokezi.

Mipango ya harusi iliandaliwa halahala ili wawili hao wafunge pingu za maisha. Hata hivyo, pasta alimwaga mtama alipokutana na kidosho steji ya bodaboda na kushauri wahudumu hao wamuige polo kwa kuoa.

“Mwenzenu mwanabodaboda anafunga ndoa takatifu na mrembo huyu. Mbona msiige mfano wake?” pasta alihoji.

“Kumbe ulinihadaa? Nisahau kabisa!” demu alikereka na kufokea jamaa kisha akazima mipango yao ya harusi.