Habari

Serikali kutumia fisi, nyani na wanyamapori wengine kulinda msitu

Na VITALIS KIMUTAI December 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI inapanga kuweka wanyamapori ndani ya msitu wa Chepalungu wenye ukubwa wa takriban ekari 12,000 katika Kaunti ya Bomet, katika jitihada za kuimarisha uhifadhi wake.

Msitu huo umegawanywa sehemu mbili – Kapchumbe yenye ukubwa wa takriban ekari 9, 884 na Siongiroi yenye takriban ekari 2,152.

Msitu huo wa kiasili umeshuhudia uharibifu mkubwa katika miongo mitatu iliyopita. Ulikuwa na miti ya kiasili ambayo ilikatwa miaka ya 1980 na jamii zinazoishi hapo karibu kwa matumizi ya nyumbani na pia wafanyabiashara wa mbao ili kuiuza, huku Shirika la Huduma kwa Misitu (KFS) likishutumiwa kwa kukosa kuchukua hatua kali na hata maafisa wake kula hongo huku uharibifu ukiendelezwa.

Hata hivyo, kampeni iliyoanzishwa na washikadau mbalimbali tangu 2015 imesaidia kubadilisha hali.

Afisa wa kulinda misitu akiwa ndani ya msitu wa Chepalungu mnamo Desemba 15, 2024. PICHA | VITALIS KIMUTAI

Kwa kawaida wanyamapori kama vile nyani, fisi na aina mbalimbali za ndege ikiwemo korongo huishi kwenye msitu huo. Japo sasa kuna mipango ya kuweka humo viumbe wengine kama vile pundamilia, ngiri na swara ambao wanaweza pia kustawi katika eneo hilo.

Kuanzishwa kwa aina nyingine za wanyama kutategemea shauri na tafiti za kitaalamu kutoka kwa Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS).

Katibu wa Kuhifadhi Wanyamapori katika Wizara ya Utalii na Wanyamapori, Dkt John Chumo, alisema serikali itahakikisha kuwa wanyama hao wanawekewa mazingira mazuri ya kuishi.

“Kuunda hifadhi ya wanyamapori katika msitu wa Chepalungu kutasaidia kudhibiti vitendo vya ukataji miti kiholela, uharibifu wa viumbe hai na uvamizi wa ardhi.  Hatua hizo tunatumai zitachangia kuundwa kwa miradi itakayotoa njia mbadala za kujikimu kwa jamii za hapo,” alieleza Dkt Chumo.

Mikakati hiyo ni katika utekelezaji wa Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori (WCMA) 2013 na Sera ya Wanyamapori 2020.

Fisi katika hifadhi ya Maasai Mara Game Reserve,Narok, awali 2017. Serikali inanuia kuongeza idadi ya fisi na wanyamapori wengine katika jitihada za kuhifadhi msitu wa Chepalungu, Bomet. PICHA | MAKTABA

“Hatua pia zitachukuliwa ili kusiwe na migogoro baina ya binadamu na wanyamapori. Pia kutakuwa na mikakati ya kuimarisha ushirikiano baina ya jamii na mashiriki ya usimamizi wa maliasili,” Katibu huyo akaongeza.

Msitu wa Chepalungu ni sehemu ya msitu pana wa Mau, ambao ni chemichemi kuu ya vyanzo vya maji ya kunywa kwa wanyama wa porini na mito inayotumiwa na binadamu.

Mito ya Mara, Sondu na Nzoia inaanzia msitu huo ambao, hata hivyo, ulishuhudia uharibifu mkubwa kwa zaidi ya miongo mitatu iliyopita.

Baadhi ya vijito katika msitu wa Chepalungu vinavyomwaga maji yazo katika Mto Mara ni Chemaetany, Kapchetirorit, Kapkibos, Atebwo, Reberwet na Legetetiet.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA