Habari za Kaunti

Mashindano ya fahali Kakamega sasa kufanyika mara tatu kwa mwaka

Na MWANDISHI WETU December 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MASHINDANO ya fahali kupigana yatakuwa yakiandaliwa kila baada ya miezi minne katika Kaunti ya Kakamega ili kuimarisha utalii katika eneo hilo, Gavana Fernandes Barasa amesema.

Bw Barasa alisema kuwa Serikali ya Kaunti imejitolea kukuza fani ya burudani katika eneo hilo kama sehemu ya nguzo yake ya kuimarisha utajiri kwa mujibu wa manifesto yake.

Alisema mashindano ya kupiganisha fahali (Mayo) ni urathi mzuri na unaokua kwa kasi ambao hutoa uzoefu usioweza kusahaulika kwa washiriki na watazamaji.

Alifichua hayo Jumanne baada ya kushiriki na kuwatunuku wamiliki wa fahali waliokuwa wakishindana wakati wa maonyesho ya mwisho wa mwaka katika uwanja wa Malinya, Ikolomani.

“Serikali yetu imejitolea kutangaza vivutio vya kipekee vya utalii kama vile mapigano ya fahali (Mayo) kama sehemu ya nguzo yetu ya uzalishaji mali.” kujenga na kuandaa viwanja vya mchezo huo katika Shinyalu, Butsoso, Malava na Khayega ili kuimarisha mchezo huo katika eneo hilo.

Maonyesho ya kupiganisha fahali yatafanyika kila baada ya miezi minne na yajayo yatafanyika Aprili mwaka ujao huko Khayega,” alisema.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na MCA wa eneo hilo Archadeous Liyayi, Rais wa mapigano ya fahali Ben Mululu miongoni mwa viongozi wengine.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA