Mbinu mpya kuimarisha upimaji kansa ya lango la uzazi
UTAFITI mpya umeonyesha kwamba uchunganuzi wa kujipima virusi vya human papillomavirus (HPV) waweza kusaidia kuainisha wanawake walio na virusi hivi katika vikundi vitatu.
Mbinu hii yaweza kusaidia kuimarisha upimaji kansa ya lango la uzazi.
Uchunguzi huo kutoka vyuo vikuu vya Karolinska Institutet na Queen Mary University of London, uliochapishwa katika jarida la PLOS Medicine, ulihusisha wanawake kutoka nchini Uingereza, waliopewa vidude vya kujipima HPV kama majaribio, kwa sababu walikuwa wamechelewa kufanyiwa uchunguzi wa kansa ya lango la uzazi.
Utafiti huo uliofanyiwa katika vituo vya afya nchini Uingereza, ulihusisha wanawake 855 waliopatikana kuwa na virusi vya HPV ambao walijipima wenyewe, na pia walifanyiwa uchunguzi mwingine na daktari.
Matokeo yalionyesha kwamba asilimia 71 ya wanawake hawa, walionyesha hatari kubwa ya kuwa na kansa, au walikuwa na kansa.
Watafiti hawa walichanganua matokeo kutoka kwa sampuli za vipimo hivyo vya kujipima na kutumia mbinu mpya kukadiria hatari kubwa ya mabadiliko ya seli.
Hatari hiyo ilitambuliwa kuambatana na aina ya virusi vya HPV na kiwango cha virusi kwenye vipimo hivyo vya kujipima.
Kisha wakawaweka wanawake hao katika vikundi vitatu: uwezekano wa juu, wastani, na chini. Wanawake waliokuwa na virusi vya HPV aina 16 walikuwa kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na kansa, au tayari walikuwa na kansa.
“Takriban asilimia 40 ya wanawake waliokuwa kwenye kikundi cha uwezekano wa juu waligundulika kuwa na hatari kubwa ya kukumbwa na kansa, au tayari walikuwa na kansa iliyohitaji matibabu. Kwa hivyo, tunapendekeza kwamba wanawake waliokuwa kwenye kikundi hiki waende kufanyiwa uchunguzi wa ukaguzi wa lango la uzazi (colposcopy) mara moja,” asema Jiayao Lei, profesa msaidizi katika Idara ya Kimatibabu ya elimu ya magonjwa na takwimu ya afya na Idara ya Sayansi ya kimatibabu, ambaye pia alikuwa kiongozi wa uandishi wa utafiti huu.
Mojawapo ya manufaa makuu ya mbinu hii ni kwamba makadirio ya hatari ya kukumbwa na maradhi haya yaweza kufanywa mara moja baada ya kupimwa virusi HPV, pasipo kuhitaji uchunguzi zaidi wa maabara.
“Hii yaweza kusaidia shughuli za kupima kansa ya lango la uzazi hasa katika mataifa maskini na yenye mapato wastani, ambapo rasilimali ni finyu,” alisema mwandishi mkuu, Peter Sasieni, Profesa katika Chuo Kikuu cha Queen Mary University of London.
Utafiti huu uifadhiliwa na mashirika ya Cancer Alliances, Cancer Research UK na the Swedish Research Council.