Museveni, Raila sasa ni chanda na pete
RAIS wa Uganda Yoweri Museveni na Kinara wa Upinzani Kenya, Raila Odinga ambao wamekuwa na tofauti kali wanaonekana kuwa na ukuruba mpya wa kisiasa, rais huyo akitarajiwa Kaunti ya Siaya Januari 2, 2025 kuadhimisha Tamasha ya Jamii ya Waluo.
Tamasha hiyo maarufu kama Piny Luo Festival itaanza Desemba 30, 2024 na kukamilika Januari 2, 2025.
Itahusisha jamii ya Waluo kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) miongoni mwa maeneo mengine ya Afrika.
Rais Museveni ataungana na mwenyeji wake Rais William Ruto kwenye kilele cha sherehe hizo ambazo ni kufunguliwa kwa uwanja wa mpya wa Jaramogi Oginga Odinga (Uwanja wa Kaunti ya Siaya) ambao una uwezo wa kusitiri mashabiki 20,000 wa soka.
Hafla hiyo imeandaliwa kwa pamoja na magavana wote wanne wa kaunti za Luo Nyanza, ambazo ni; Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori.
Jiji la Kisumu ndilo huzingatiwa kama makao makuu ya Waluo kutoka mataifa mbalimbali Afrika.
Mnamo Jumatatu, Desemba 23, 2024 Bw Odinga akizungumza katika eneobunge la Bondo kwenye hafla iliyoandaliwa na mwanasiasa wa ODM Andiwo Mwai, alitoa wito kwa Waluo wajitokeze kwa wingi na kumkaribisha Rais Museveni.
“Kila mara tumekuwa na tabia nzuri ya kuwakaribisha wageni wanaotutembelea. Nawaomba watu wetu wajitokeze kwa wingi na kumkaribisha Rais Museveni na wageni wote watakaokuja hapa,” akasema Bw Odinga.
“Wanakuja hapa kufahamu mila, tamaduni na desturi yetu na tunastahili kuonyesha ulimwengu wote kuwa sisi ni watu karimu wenye umoja,” akaongeza Bw Odinga.
Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye alikuwa akiongea kwa Kiluo, pia aligusia siasa ambapo aliitaka jamii ya Waluo isalie dhabiti ndani ya ODM kwa kuwa ndiyo silaha yao katika siasa za nchi.
“ODM ni chama chetu na ndiyo silaha yetu, hata nikishiriki siasa za Afrika chama lazima kiwe imara na kilindwe kwa hali yoyote ile,” akasema.
Kuimarisha maandalizi ya Rais Museveni na Rais Ruto Siaya, Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Raymond Omollo alitembelea Kaunti ya Siaya Jumatatu, akazuru uwanja ambao utafunguliwa na kuandaa mazungumzo na Gavana James Orengo.
“Rais Museveni, Rais Ruto na Mheshimiwa Raila Odinga pamoja na wageni wengi wakuu watakuja. Raila ni mwenyeji wa hapa, Afrika Mashariki na Afrika itakuwa wakati wa kusherehekea utamaduni wa Waluo,” akasema Bw Omollo.
“Tunapania kukaribisha wageni wote. Ni wakati wa kuonyesha umoja wetu na tujiandae kukaribisha watu wote tuwaonyesha tamaduni zetu,” akaongeza Bw Omollo.
Gavana Orengo naye alisema kuwa maandalizi yote yamekamilika na akatoa wito watu wajitokeze kumkaribisha Marais Museveni, Ruto na Raila pamoja na wageni wengine.
“Nawakaribisha Wakenya wote na Waluo wote kwa sababu ni wakati wa kusherehekea na kujivunia utamaduni wetu, historia na lugha yetu,” akasema Gavana huyo.
Ujio wa Rais Museveni Siaya unakuja wakati ambapo kiongozi huyo amekuwa mstari wa mbele kumpigia debe Bw Odinga kwenye nia yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
“Kijana kutoka Djibouti alikuja na akaniambia yeye ndiye mwaniaji wao. Tulipiga gumzo, picha na kunywa chai. Lakini nilimwaambia peupe nitaenda Kenya kumuunga Raila kwa sababu ndiye anatosha kwa kazi hii,” akasema Rais Museveni mnamo Agosti 27, 2024 katika Ikulu ya Nairobi wakati wa uzinduzi wa azma ya Raila.
Alikuwa akirejelea Mahamoud Youssouf ambaye anawania uenyekiti wa AUC na pia ni mpinzani mkuu wa Bw Odinga kwenye kura hiyo ya Februari 2024.
“Raila hatafuti kazi hii kwa sababu ya maslahi yake ya kibinafsi, bali anatosha na ni mwana taaluma ambaye ameonyesha sifa nzuri ya uongozi,” akaongeza Rais Museveni.
Kiongozi huyo aliwapatanisha Raila na Rais Ruto mnamo Februari 26 mwaka huu baada ya kukutana nao nyumbani kwake Kisozi, Uganda.
Wawili hao waliridhiana na hata Bw Odinga akamwokoa Rais kwa kuwaruhusu wanachama wa ODM kuingia serikalini wakati wa kilele cha maandamano ya Gen Z mnamo Julai mwaka huu.
Maandamano hayo ya vijana yalitishia kuangusha utawala wake.
Ukuruba wa Rais Museveni umeshamiri japo miaka ya nyuma, wawili hao wamekuwa na tofauti kali wala hawakuwa wakionana uso kwa macho.
Baada ya uchaguzi wa 2007, Museveni aliwalaumu wafuasi wa Raila mtaani Kibera kwa kung’oa reli na kusambaratisha uchukuzi wa bidhaa hadi Uganda.
Wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017 na maandamano, kulikuwa na madai ambayo yalikanushwa kuwa Uganda ilikuwa ikishirikiana na utawala wa Jubilee kuleta polisi maeneo ya Nyanza kuwakabili waandamanaji.
Mzozo kati ya wavuvi kisiwani Migingo ni kati ya masuala ambayo yanadaiwa yamekokota kupata suluhu kutokana na tofauti za kisiasa kati ya Raila na Rais Museveni.
Wavuvi kutoka Kenya wamekuwa wakilalamika kuhangaishwa na polisi kutoka Uganda huku wakikamatwa na kuzuiliwa kisha kuachiliwa baada ya kutozwa faini kubwa.
Mwaka 2015, Rais Museveni na Raila walijibizana vikali wakati ambapo Bw Odinga alipinga kuingizwa kwa sukari kutoka Uganda hapa nchini Kenya na kuendesha misururu ya mikutano kuhusu suala hilo Nyanza na Magharibi.
Rais Museveni alimshutumu vikali kwa hatua hiyo naye Bw Odinga akamwaambia akome kuingilia masuala ya ndani ya Kenya.