Jamii ya Suba yataka lugha yao ifundishwe shuleni
JAMII wa Suba sasa inaitaka serikali kujumuisha lugha ya Olusuba katika mfumo wa elimu ili kuwawezesha watoto kuisoma katika umri mdogo.
Mtafsiri wa lugha ya Olusuba Victor Warekwa alisema wanashirikiana na Wizara ya Elimu kuiweka lugha hiyo kuwa miongoni mwa lugha zinazofundishwa shuleni.
Alisema wametafsiri vitabu vya Biblia katika agano la kale kwa lugha hiyo.
Jamii hiyo sasa inahisi kuwa lugha hiyo inapotea hasa miongoni mwa vijana wa Gen Z, kwani baadhi wanaiga mtindo wa kisasa.
“Watoto kujifunza lugha ya kiasili ni mojawapo ya njia bora zaidi kuhakikisha kuwa utamaduni na lugha hiyo inapitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine,” Bw Warekwa alisema.
Narkiso Okello, mmoja wa wazee anayesimamia maandalizi ya tamasha ya kila mwaka ya kufufua lugha yao anasema kuwa japo wana lugha yao ya kiasili, baadhi ya wanajamii hawawezi kuzungumza na hawaelewi Olusuba, lugha inayozungumzwa na Abasuba.
Wengi wao wanajitambulisha kama “Subanese” lakini hawaelewi wala hawana ufahamu kuhusu tamaduni zao.
Badala yake, wanazungumza Dholuo kwa ufasaha na kuwaacha wazee waking’ang’ana na lugha yao ya kiasili.
Hili ni jambo la kusikitisha sana kwa wazee kutoka katika jamii.
Bw Okello, alisema vijana na watoto kutoka jamii wanazidi kutelekeza utamaduni wao wakiiga mitindo ya kisasa.