Kimataifa

Ndege iliyokuwa na abiria 69 yaanguka Krismasi

December 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NDEGE ya abiria aina ya Embraer iliyokuwa ikitoka Azerbaijan kwenda Urusi ilianguka karibu na mji wa Aktau huko Kazakhstan siku ya Jumatano ikiwa na abiria 62 na wafanyakazi watano, maafisa waKazakhstan walitangaza, wakisema kuwa watu 28 walinusurika.

Video ambayo haijathibitishwa ya ajali hiyo ilionyesha ndege hiyo ya shirika la ndege la Azerbaijan Airlines, ikiwaka moto huku ikianguka chini na moshi mzito mweusi kupaa. Abiria waliotokwa damu na waliojeruhiwa walionekana wakijikwamua kutoka kipande cha mabaki ya ndege hiyo.

Wizara ya dharura ya Kazakhstan ilisema katika taarifa kwamba huduma za zima moto zilizima moto huo na kwamba walionusurika, wakiwemo watoto wawili, walikuwa wakitibiwa katika hospitali iliyo karibu. Miili ya waliofariki ilikuwa ikitolewa.

Shirika la ndege la Azerbaijan lilisema ndege hiyo aina ya Embraer 190, yenye nambari ya J2-8243, ilikuwa ikitoka Baku hadi Grozny, mji mkuu wa eneo la Chechnya nchini Urusi, lakini ililazimika kutua kwa dharura karibu kilomita 3 (maili 1.8) kutoka Aktau nchini Kazakhstan. Jiji hilo liko kwenye mwambao wa Bahari ya Caspian kutoka Azerbaijan na Urusi.

Mamlaka nchini Kazakhstan zilisema tume ya serikali imeundwa kuchunguza kilichotokea na wanachama wake waliamriwa kusafiri kwa ndege hadi eneo hilo na kuhakikisha kuwa familia za waliokufa na waliojeruhiwa zinapata msaada zinaohitaji.

Kazakhstan itashirikiana na Azerbaijan katika uchunguzi, serikali ilisema.

Shirika la uangalizi wa anga la Urusi lilisema katika taarifa yake kwamba taarifa za awali zilidokeza kwamba rubani aliamua kutua kwa dharura baada ya kugonga ndege.

Kufuatia ajali hiyo, Ilham Aliyev, rais wa Azerbaijan, alirejea nyumbani kutoka Urusi alikokuwa akihudhuria mkutano wa siku ya Jumatano, shirika la habari la Urusi la RIA liliripoti.

Ramzan Kadyrov, kiongozi wa Chechnya anayeungwa mkono na Kremlin, alituma rambirambi katika taarifa na kusema baadhi ya wale wanaotibiwa hospitalini wako katika hali mbaya sana na kwamba yeye na wengine wanawaombea wapone haraka.